Dar es Salaam. Katika kukabiliana na utegemezi wa bidhaa za soya kutoka nje ya nchi, Tanzania imeanza kuhamasisha uwekezaji unaolenga kuchochea ukuaji wa sekta hiyo kupitia uchakataji wa kisasa, masoko yaliyopangiliwa, na ushiriki mpana wa wakulima.

Sekta ya soya nchini bado iko katika hatua za awali za maendeleo, ikiwa na uzalishaji unaokadiriwa kuwa chini ya tani 30,000 kwa mwaka, wakati mahitaji ya ndani yanaongezeka kwa kasi, yakichochewa na viwanda vya chakula cha mifugo na uzalishaji wa mafuta ya kula.

Katika kukabiliana na hilo,Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) Kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe, kampuni ya Mount Meru Millers Limited (MMM), pamoja na mshirika wa maendeleo Gatsby Africa, COPRA imefanya majadiliano kuhusu uwekezaji mkubwa unaolenga kukuza sekta ya soya nchini.

Akizungumza baada ya majadiliano yaliyofanyika mkoani Songwe leo, Aprili 20, 2026, Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, amesema upungufu uliopo umechochea ongezeko la uagizaji wa bidhaa za soya kutoka nje ya nchi, hali inayodhoofisha ushindani wa sekta muhimu kama vile ufugaji wa kuku, samaki na mifugo kwa ujumla.

“Kupitia majadiliano na uwekezaji huu, tunaona Mkoa wa Songwe ukitoa eneo la uwekezaji kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kuchakata na kusafisha soya,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa za soya kutoka nje, huku ikiimarisha uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula na malighafi za chakula cha mifugo.

“Uwekezaji huo unatarajiwa kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakulima wadogo na kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali zinazotegemea soya,” amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa COPRA, Irene Mlola, wa pili kutoka kushoto akiwa na baadhi ya wadau wa zao la Soya.

Amesema utofauti wa uwekezaji huo utakaofanywa na kampuni ya Mount Meru Millers Ltd utajikita katika mfumo wa soko unaomlenga mkulima moja kwa moja, ukiwemo upatikanaji wa soko la uhakika, mifumo ya ununuzi iliyo wazi, na bei zitakazojulikana mapema.

“Kupitia mikataba ya kilimo, wakulima na vikundi vyao watanufaika na bei ya uhakika itakayowekwa kabla ya msimu wa kilimo. Hatua hii itawawezesha kupanga uzalishaji wao, kupata pembejeo kwa uhakika, na kupunguza hatari ya mabadiliko ya bei,” amesema.

Amesema wakati wa mavuno, wakulima watanufaika pia na bei za soko endapo zitakuwa juu zaidi, jambo litakalolinda kipato chao na kuwapa nafasi ya kunufaika na ongezeko la bei.

“Uwekezaji huu hauhusu tu ujenzi wa kiwanda, bali pia kuanzishwa kwa mfumo wa soko ulio wazi na unaotabirika kwa wakulima wetu. Kwa kuhakikisha upatikanaji wa soko la uhakika na kuweka mifumo ya bei iliyo wazi, tunawapa wakulima ujasiri wa kuongeza uzalishaji huku taifa likinufaika na ongezeko la thamani na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje,” amesema.

Amesema Mamlaka hiyoitaendelea kuwezesha uwekezaji wa sekta binafsi wenye uwajibikaji, huku ikihakikisha mifumo ya udhibiti inalinda maslahi ya wakulima na wadau wote katika mnyororo wa thamani, kukuza uwazi, na kuchochea ukuaji endelevu wa sekta.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *