Ni katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, ‘Madini! Maisha na utajiri’ ndio kauli inayosikika. Wachimbaji wadogo, wataalamu wa madini, taasisi za kifedha na viongozi wa serikali wamekutana. Dhumuni kubwa, kuleta mageuzi katika sekta ya madini yasiyopewa kipaumbele hususan ya ujenzi ikiwemo chokaa, jasi, na mawe, ili yaweze kumkomboa mwananchi kiuchumi.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza usalama kazini na tija kwa kutumia mbinu za kitaalamu za uandaaji wa mashimo, uongezaji wa thamani ya madini, na kuunda vyama vya ushirika ili kukuza mitaji yao. Mhandisi Migodi na Mkaguzi wa Migodi na Baruti kutoka Ofisi ya Madini mkoani Singida, Mhandisi Lameck Maduhu, anaeleza.

“Mada kubwa ambayo tulikuwa tukiizungumzia ni kuhusiana na kuimarisha usalama, afya pamoja na mazingira katika maeneo yao ya uchimbaji. Kama tujuavyo kwamba katika shughuli za uchimbaji zimekuwa kwenye mazingira ambayo yana vihatarishi vingi na ajali nyingi zimekuwa zikitokea maeneo hayo na kugharimu maisha ya watu nap engine kusimamisha shughuli za uchimbaji na uchumi kusimama kulingana na shughuli hizo kusimama.”

Mwanamume aliyevaa shati lenye mistari anawasilisha hotuba kwenye mkutano kuhusu uchimbaji madini nchini Tanzania. Bendera kubwa nyuma yake inaonyesha nembo za UNDP, ACP-EU Development Minerals Programme, na Umoja wa Ulaya, pamoja na maandishi ya Kiswahili.

UNDP yatoa mafunzo ya kuimarisha ujuzi wa uchimbaji salama wa madini kwa wanawake na vijana wanaojihusisha na uchimbaji mdogo wa madini ya ujenzi Tanzania.

Mratibu na mtaalam wa masuala ya jinsia wa UNDP, Clara Maliwa amesema wanatamani kuona vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu wanashika nafasi za juu zaidi ikiwemo, kumiliki kampuni na kutoa ajira kwa wengine badala ya kuwa vibarua.

Baada ya mafunzo, wachimbaji wameelimika, Eva Ngoma, mchimbaji wa madini ya jasi au gypsum anaeleza.

“Nimeelewa kwamba uchimbaji wangu haukuwa salama, kwasababu unachimba madini ya jasi, unaacha kifusi juu, chini unaona kuna maji kwa hiyo unaona gharama kushusha kifusi kutoka kule juu, lakini kutokana na mfunzo ya jana nimeelewa kuwa kumbe ni bora nikapunguza kile kifusi ili nichimbe kwa usalama.”

Naye, Fatuma Alimasi, mchimbaji wa madini ya chumvi, ameahidi kuisambaza elimu hiyo kwa wengine.

“Mafunzo niliyoyapata, nitakaporudi nitaweza kuwafundisha wenzangu kufuata yale tuliyofundishwa, tubadilike na yale mazingira tuliokuwa nayo.”

Mradi huu ni mwendelezo wa juhudi za UNDP nchini Tanzania kuhakikisha ukuaji jumuishi wa kiuchumi unawafikia wale walio pembezoni, matokeo yanaonekana kwani Serikali imeshazindua maeneo mapya sita ya uchimbaji na kutoa leseni 1,279 mkoani Singida, huku ushiriki wa wanawake na vijana ukiongezeka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *