
Rais wa Iran na Spika wa Bunge wametoa kauli tofauti wakiahidi kuwajibisha tawala katili za Marekani na Israel kwa mauaji ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, huku maafisa wa ngazi za juu kutoka zaidi ya nchi 30 wakikusanyika Tehran kwa ajili ya shughuli za mazishi zinazotarajiwa kuvutia hadi waombolezaji milioni 20.
Rais Masoud Pezeshkian amesema leo Ijumaa kuwa Tehran itaendeleza hatua za kisheria na kidiplomasia dhidi ya Marekani na Israel kwa “uvunjaji dhahiri” wa sheria za kimataifa, huku Spika Mohammad Bagher Qalibaf akiambia ujumbe wa Lebanon kwamba “kulipiza kisasi cha damu” ya Kiongozi kunamaanisha kuwakomboa Waislamu wote wanaokandamizwa na Marekani na Israel.
Rais Pezeshkian alitoa matamshi hayo wakati wa vikao vyake tofauti na wajumbe maalum kutoka China, Namibia na Afghanistan waliofika Tehran kuhudhuria shughuli za mazishi.
Rais WA Iran amesema: “Vitendo vilivyofanywa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilikuwa uvunjaji wa wazi wa misingi ya Kifungu cha Msingi cha Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa ambazo ni lazima kutekelezwa, kanuni ya kuheshimu mamlaka ya kitaifa, na viwango vyote vya sheria za kimataifa za kibinadamu.”
Rais Pezeshkian amesema Iran itafuatilia uhalifu huo na kuwawajibisha wahusika na wale waliowaunga mkono katika majukwaa na taasisi za kimataifa, ikitumia uwezo wake wote wa kisheria na kidiplomasia.
Amesisitiza kuwa Iran imejizatiti kuimarisha uhusiano na majirani zake kwa misingi ya ujirani mwema, kuheshimiana, na maslahi ya pamoja.
Ameongeza kuwa: “Hakuna nchi inapaswa kuruhusu ardhi yake, miundombinu yake, au uwezo wake kutumiwa na wachokozi dhidi ya taifa la Iran.”
Katika kikao tofauti, Qalibaf alipokea ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Harakati ya Amal ya Lebanon ukiongozwa na Khalil Hamdan, aliyemwakilisha Spika wa Bunge la Lebanon Nabih Berri na kuwasilisha ujumbe wa maandishi kutoka kwake.
Qalibaf amesema: “Bila shaka, kulipiza kisasi cha damu ya kiongozi mkuu kama huyu kunamaanisha kuwakomboa Waislamu wote dhidi ya ukandamizaji wa Marekani na utawala wa Kizayuni.”
Qalibaf, ambaye ni mwenyekiti wa timu ya mazungumzo ya Iran katika mazungumzo ya upatanishi ya Pakistan kati ya Iran na Marekani, amesema moja ya masuala muhimu katika Hati ya Makubaliano ya Islamabad kati ya Iran na Marekani ilikuwa mustakabali wa Mhimili wa Muqawam, hususan Lebanon.
Qalibaf amebainisha kwamba Iran ilisisitiza kujumuisha vifungu vinavyohusu Lebanon katika makubaliano hayo yenye vipengele 14 yaliyosainiwa katikati ya Juni, ambayo yalitangaza kusitishwa kwa mara moja na kwa kudumu kwa operesheni zote za kijeshi katika medani zote.
Shughuli za mazishi zilianza Ijumaa ambapo mwili wa Shahidi Ayatullah Khamenei uliwekwa hadharani katika Ukumbi wa Mosalla jijini Tehran. Baada ya hapo, mwili utasafirishwa kuelekea mji wa Qom, kisha kwenda miji mitakatifu ya Najaf na Karbala nchini Iraq, kabla ya maziko mnamo Julai 9 katika haram ya Imam Ridha (AS) huko Mashhad kaskazini mashariki mwa Iran, mahali alipozaliwa Shahidi Imam Khamenei.
Maafisa wa ngazi za juu na wawakilishi kutoka zaidi ya nchi 30, zikiwemo Russia, China, Pakistan, India, na nyinginezo, wamewasili Tehran kuhudhuria shughuli hizo.
Wajumbe wa China, Namibia na Afghanistan, katika mazungumzo yao na Rais Pezeshkian, walitoa salamu za rambirambi kutoka kwa viongozi wao, wakasisitiza kuheshimu mamlaka ya Iran na mipaka yake, na wakatoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kitamaduni, na maeneo mengine mbalimbali.