DUNIA ya soka kuna walinzi wagumu ambao hadi kuwapita unatakiwa ufanye kazi kubwa, la sivyo kama wewe ni mshambuliaji basi utaonekana huna maana yoyote.

Katika hilo, kuna wachezaji wanatumia mbinu mbalimbali za kuwapita mabeki ili kufunga mabao, huku mshambuliaji wa JKU, Feisal Hilali Nassor akiwa na siri ya kukabiliana na mabeki wagumu, licha ya kukiri kwamba bado kuna wawili wanamsumbua zaidi ndani ya Ligi Kuu Zanzibar.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ambaye licha ya safari yake kisoka kuwahi kukumbwa na changamoto ya kutopewa nafasi kutokana na mvutano na kocha, lakini anasema hakukata tamaa, akaendelea kupambana hadi leo ni mmoja wa wachezaji muhimu.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, Feisal amezungumza mambo mengi ya ndani na nje ya uwanja ikiwemo changamoto alizokutana nazo huku kubwa zaidi akibainisha kwamba bado matamanio yake ni kuona anarudi kucheza Ligi Kuu Bara baada ya kuachana na Kagera Sugar 2023 ambapo alikuwa hapo tangu 2019. Kwa sasa Kagera Sugar inashiriki Ligi ya Championship baada ya kushuka daraja msimu wa 2024-2025.

Akizungumzia kilichomkwamisha ndani ya Kagera Sugar hadi anaondoka, Feisal anasema: “Nilishawahi kuichezea Kagera Sugar na kitu ambacho kilinikwamisha ni walimu, licha ya juhudi zangu bado sikufanikiwa kuendelea kusalia kikosini hapo, nikarudi Zanzibar kuangalia bahati nyingine.”

Anasema kwake ilikuwa changamoto kubwa kuona anaendelea kupambana lakini anarudishwa nyuma na walimu waliokuwa kama hawamuoni anachokifanya.

Nyota huyo anabainisha kwamba, hali hiyo imekuwa ikiwatokea wache zaji wengi na hata sasa ndani ya Ligi Kuu Zanzibar kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakilalamikia suala hilo.

Anafichua kwamba, ishu hiyo mara nyingi hutokea pale ambapo mchezaji anapomkosea kocha, basi kosa hilo hutumika kama sehemu ya adhabu, huku akiomba isiwe hivyo na badala yake kuwekwa chini na kupewa maelekezo ya nini cha kufanya kwani makocha ni kama wazazi kwa wachezaji.

Feisal anasema, sehemu alipo sasa ndani ya kikosi cha JKU, anaona ni salama zaidi kwani klabu hiyo imekuwa na kawaida ya kuwapa nafasi kubwa vijana kuonyesha uwezo wao kama ilivyokuwa kwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Abubakar Nizar ‘Ninju’ ambao wote wametokea hapo kabla ya kusaini Yanga.

Alianza Fei Toto kutoka JKU na kutua Yanga mwaka 2018 wakati ana miaka 20, kabla ya 2023 kuhamia Azam alipo sasa, kisha Ninju naye 2025 akatua Yanga akiwa na miaka 16, huku nyota hao wote wakiondoka Zanzibar wakiwa na umri mdogo.

MBINU ZA KUPENYA WALINZI

Ili uwe mshambuliaji hodari, huna budi kuwa na mbinu bora ya kuipenya ngoma ya ulinzi ya wapinzani kitu ambacho Feisal anasema kwake mbinu kubwa anayoitumia ni kucheza na akili ya beki kwa kumuangalia udhaifu wake.

Anaeleza kwamba, anapofanikiwa kumsoma beki wa timu pinzani, inampa urahisi wa kutumia mitindo tofauti na kupenya kati yake.

Anasema, nafasi za kufunga huwa ni chache sana, hivyo zinazopatikana kwenye mechi huitumia vizuri ili asipoteze matumaini kwa timu yake.

Mshambuliaji huyo ambaye katika ufungaji wake, anapendelea zaidi kutumia mguu na sio kichwa akiamini kwamba mtindo huo anauona kwake ni rahisi zaidi, anasema kabla ya mechi kuanza huwa anasisitizwa na kocha wake kutumia nguvu na spidi ili kuimarisha uwezo wake.

MBONDE, CARRAGHER MABEKI WAGUMU

Licha ya kwamba amekuwa akiitumia mbinu hiyo kufanikiwa, lakini kati ya mabeki ambao wanampa tabu katika Ligi Kuu ya Zanzibar ni wa Muembe Makumbi, Samir Carragher na Salim Mgaya ‘Mbonde’ anayecheza KVZ, akibainisha kwamba mabeki hao wanatumia akili na nguvu.

Anafichua kwamba: “Ili umpite beki anayetumia akili na nguvu, basi inakupasa utumie akili nyingi zaidi sambamba na kuwa mtulivu na kufanya uamuzi wa haraka, kinyume na hapo huwezi kufanikiwa.”

ANAVYOKABILIANA NA PRESHA YA MASHABIKI

Anasema: “Katika mchezo hakuna siku nzuri pekee, lazima na mbaya itakuwepo, hivyo presha ya mashabiki inatokea pale ambapo unategemewa lakini kumbe sio siku yako, pengine umeamka vibaya, hivyo unapaswa kutambua hilo.

“Ikitokea hali hiyo, inabidi nifanye kazi mara mbili ili kuipa timu ushindi na kuwaridhisha mashabiki wangu.”

Anasema wachezaji wengi wanatoka mchezaji wanapokosa nafasi ya wazi ya kufunga kisha wakapokea maneno kutoka kwa mashabiki, lakini kwake ikitokea hivyo, anatumia muda huo kujituliza kisaikolojia kwa lengo la kutengeneza nafasi nyingine kuwasahaulisha mashabiki alichokikosa na kufurahia aliyopata.

NEYMAR, RONALDO WANAMKOSHA

Feisal anasema anavutiwa zaidi na nyota wa Brazil, Neymar na anapenda namna ya uchezaji wake ingawaje hautumii sana.

Kwa upande mwingine, anamkubali Cristian Ronaldo wa Ureno kwa namna anavyofunga mabao akiwa uwanjani na muda mwingi anautumia kuangalia video zake kwa ajili ya kujifunza.

NDOTO ZA BUNDESLIGA

Mbali na matamamanio yake ya kurudi Ligi Kuu Bara, Feisal mwenye mabao manne na asisti tano katika mechi 14 za Ligi Kuu Zanzibar msimu huu, anasema katika maisha yake ya soka anatamani siku moja kupata nafasi ya kuichezea Ligi Kuu ya Ujerumani ‘BUndesliga’ kwani ikiwa hivyo, atakuwa amefikia nusu ya ndoto zake.“Naipenda Ligi ya Ujerumani kwasababu mpira wake sio mgumu sana kama ilivyo nchi nyingine, pia navutiwa na mji wake ulivyotulia,” anasema.

UJUMBE WAKE

Anamaliza kwa kutoa wito kwa vijana wanaotamani kuwa kama yeye akisema: “Wanapaswa kujiamini, kusimama imara na kutimiza ulichopewa kwa moyo wote kwa sababu wanaokuamini wanaona uwezo uliopo ndani yako hata wakati ambao wewe huujui vizuri.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *