
Nigeria. Baada ya msanii wa Nigeria Peter Okoye ‘Mr P’ aliyekuwa kwenye kundi la P-Square kubadilisha tarehe ya kuzaliwa ili isifanane na ya pacha wake, mashabiki wamemjia juu wakitaka aache kutumia jina la P-Square.
Kupitia mtandao wa X baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiandika Peter anapaswa kuacha kutumia jina la ‘P-Square’ kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii, ikiwa kweli ana nia ya kujitenga na kaka yake.
Kutokana na mjadala huo ambao unaendelea katika mitandao ya kijamii Mr P, alijibu akieleza haoni sababu ya kuacha kutumia jina hilo. Akisisitiza yeye ndiye aliyelianzisha na kulifanya lijulikane, hivyo ana haki ya kulitumia.
“Mimi ndiye niliyegundua jina hilo, hivyo nitaendelea kulitumia,”aliandika katika ukurasa wake wa X
Mbali na hilo aligusia kuhusu chanzo cha mgogoro na pacha wake. Akidai alisalitiwa na ndugu zake katika masuala ya kifamilia na kibiashara yaliyohusu uendeshaji wa kazi zao za muziki.
Hata hivyo, alikanusha madai ya kwamba mke wa mmoja wa ndugu zake aliwahi kuwashauri kumwibia. Akifafanua kuwa wakati wa madai hayo hakuna hata mmoja wao ambaye alikuwa ameoa.
Ikumbukwe mapema wiki hii Mr P alitangaza kubadilisha tarehe ya kuzaliwa na kuwa hatopokea zawadi wala ujumbe wowote siku ambayo awali waliisherekea pamoja na kaka yake.
“Ninapenda kuwajulisha rasmi kuwa ninabadilisha tarehe ya kusherehekea siku yangu ya kuzaliwa. Kuanzia sasa, Novemba 18 haitakuwa tena siku yangu ya kusherehekea birthday. Tafadhali tambueni kwamba sitapokea ujumbe wala zawadi zozote siku hiyo.
“Kuanzia sasa, siku yangu ya kuzaliwa itakuwa inaadhimishwa Novemba 30. Huu ni uamuzi binafsi, na ninathamini sana uelewa wenu.”
Licha ya kinachoendelea katika mitandao ya kijamii pacha wa mwanamuziki huyo Paul Okoye hajazungumza chochote hadi sasa kuhusiana na uamuzi wa ndugu yake kubadili tarehe ya kuzaliwa.