Dar es Salaam. Hatimaye pazia limeanza kufunguliwa kuhusu chanzo, madhara na waliokuwa nyuma ya ghasia zilizotikisa nchi wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025, baada ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani kuwasilisha ripoti yake.

Akiwasilisha ripoti hiyo leo, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Othman Chande amesema uchunguzi huo ulilenga kutoa picha halisi ya matukio hayo pamoja na kuweka msingi wa kuzuia yasijirudie.

Jaji Chande amesema kazi hiyo ilihusisha ukusanyaji mpana wa taarifa kutoka kwa waathirika na wadau mbalimbali, hatua iliyoiwezesha tume kupata taswira ya kina ya kilichotokea.

Amesema jukumu kuu la tume hiyo lilikuwa kubaini ukweli kuhusu matukio ya ghasia yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa 2025.

Amesema hadidu za rejea, tume ilichunguza chanzo halisi cha ghasia zilizotokea siku ya uchaguzi na siku chache zilizofuata, pamoja na kubaini malengo ya waliohusika katika kupanga na kutekeleza vitendo vya uvunjifu wa amani.

Aidha, ilichambua madhara yaliyotokana na matukio hayo, ikiwemo vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na miundombinu, pamoja na athari za kiuchumi na kijamii.

Tume pia ilichunguza mazingira na hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na ghasia hizo, sambamba na kutoa mapendekezo ya namna ya kuimarisha uwajibikaji wa viongozi na wananchi katika kulinda amani, kuheshimu utawala wa sheria na haki za binadamu.

Mapendekezo hayo yanahusisha pia kuimarisha utawala bora na kukuza majadiliano ya kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa lengo la kufikia maridhiano ya kitaifa na kuzuia kujirudia kwa matukio kama hayo.

Katika utekelezaji wake, tume ilifanya uchunguzi katika maeneo 202 yaliyoathirika zaidi katika wilaya 21 za mikoa 11 ikiwemo Dar es Salaam, Geita, Mbeya, Songwe, Mwanza, Arusha, Iringa, Dodoma, Shinyanga, Mara na Ruvuma.

Aidha, ilitembelea Zanzibar na Mkoa wa Kilimanjaro kama sampuli ya maeneo ambayo hayakukumbwa na ghasia, kwa lengo la kujifunza sababu zilizosaidia kudumisha amani.

Kwa upande wa ukusanyaji wa taarifa, jumla ya waathirika 1,323 walisikilizwa, huku maelezo ya kiapo yakichukuliwa kwa waathirika 553.

Tume pia ilipokea mawasilisho ya maandishi 159 kupitia posta, 323 yaliyowasilishwa moja kwa moja ofisini na 557 kupitia barua pepe.

Mbali na hayo, madodoso 4,891 yalipokelewa, pamoja na jumbe fupi 33,250 na jumbe za WhatsApp 23,195.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *