Dodoma. Watoto watatu wenye umri kati ya miaka mitano na sita wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye bwawa la kuogelea lililopo ndani ya hoteli ya Esperanza, inayofanyiwa ukarabati katika eneo la Swaswa, jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gallus Hyera, watoto hao walikuwa wanafunzi wa darasa la awali. Inadaiwa waliingia katika eneo la hoteli hiyo isiyokuwa na ulinzi, wakitokea shuleni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Aprili 23, 2026, Kamanda Hyera amesema wanafunzi hao waliruhusiwa kurejea nyumbani saa tano asubuhi, lakini hawakufika makwao kama ilivyotarajiwa.

Badala yake, inaelezwa kuwa walielekea katika hoteli hiyo, na walivua nguo na kuweka mabegi pembeni kabla ya kuingia kwenye bwawa la kuogelea.

“Wanafunzi hao waliruhusiwa kurudi nyumbani saa tano asubuhi, lakini hawakufika. Ilipofika saa 12 jioni ndipo tulipokea taarifa ya tukio hili. Tulipofika eneo la tukio, tulibaini kuwa ni kweli watoto hao watatu walikuwa wamefariki dunia baada ya kuzama kwenye bwawa hilo,” amesema Kamanda Hyera.

Ameongeza kuwa hadi sasa hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo. Pia ameeleza kuwa walinzi waliopaswa kuwepo eneo la hoteli hiyo hawakuwepo, huku mmiliki wa hoteli hiyo, anayetajwa kwa jina moja la Maendeleo, bado hajapatikana.

Kamanda Hyera amesema uchunguzi unaendelea ili kubaini kwa kina mazingira ya tukio hilo pamoja na utambulisho kamili wa mmiliki wa hoteli hiyo.

Aidha, ametoa wito kwa wamiliki wa hoteli na maeneo mengine ya huduma kuhakikisha wanaimarisha ulinzi na usalama kwa watu wanaoingia na kutoka katika maeneo yao.

“Anaweza kuwa watoto hawa waliwahi kufika hapo awali wakiwa na wazazi wao chini ya uangalizi, lakini safari hii hali ilikuwa tofauti na kusababisha madhara makubwa,” amesisitiza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *