
Dar es Salaam. Zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa lililotangazwa jana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi limeibua mambo mapya baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kusisitiza hakuna haja ya kubishana kuhusu suala hilo, badala yake washughulikie usalama wa nchi, Watanzania na rasilimali za Taifa.
Wakati Dk Mwigulu akieleza hayo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitajifungia kwa siku nne kujadili hali ya kisiasa likiwemo zuio hilo, huku ACT Wazalendo ikitangaza kusudio la kwenda mahakamani kulipinga.
Jana Juni 26, 2026, Waziri Katambi alitangaza bungeni zuio la mikutano ya vyama vya siasa kwa kile alichoeleza kuwa ni kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani katika kipindi cha Maonyesho ya Kibiashara ya Sabasaba.
Uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya watu wakihamasisha kufanya maandamano kwenye mitandao ya kijamii, wakitaka yafanyike siku ya Julai 7, ambayo ni maalumu kwa maonyesho ya kibiashara nchini, kila mwaka.
Hii ni mara ya pili Serikali kuweka zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa. Mara ya kwanza lilitangazwa mwaka 2016 chini ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tano, hayati John Magufuli, kabla ya kuondolewa na Rais Samia Suluhu Hassan Januari 3, 2023.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa zuio la mwaka 2016, uamuzi wa sasa umekosolewa na wadau wa siasa na sheria, waliosema unakwenda kinyume na Ibara ya 20(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Vyama vya siasa na Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi.
Msisitizo wa Mwigulu
Akiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo, Juni 27, 2027 huko Ikungi mkoani Singida, Dk Mwigulu amesisitiza kwamba kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kuhakikisha usalama wa wananchi na rasilimali za taifa unalindwa dhidi ya watu waliopanga kufanya vurugu.
Amesema mambo yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana ambayo yaliumiza watu wengi, yanataka kujirudia na yameanza kuonekana kwa njia zilezile, jambo ambalo hawataruhusu litokee tena na hawatacheka na wahusika.
“Ndugu zangu Watanzania, wala tusibishane kuhusu mikutano ya vyama vya siasa, hiyo ipo kikatiba, hiyo ipo tu. Sasa hivi tushughulikie suala la usalama wa nchi yetu, usalama wa Watanzania na usalama wa haohao walioko kwenye vyama vya siasa,” amesema.
Amesisitiza kwamba Serikali haina ugomvi na chama chochote cha siasa, lakini kuna jambo la kipaumbele la usalama wa nchi, Watanzania na rasilimali za nchi.
Dk Mwigulu amesema moja ya mambo ambayo hawana mzaha nayo ni kuhusu ulinzi wa nchi, ulinzi wa Watanzania na ulinzi wa rasilimali za Tanzania.
Amesema hayo si mambo ya mzaha wala hayana upande, yanawahusu Watanzania wote.
“Tanzania ina vyama vya siasa, lakini vyama hivi vipo tu kwa sababu kuna Tanzania. Hata dini zetu, tunaweza kufanya ibada kama kuna amani, pakichafuka hakuwezi kufanya ibada, ulizeni zile nchi wanazopigana kila siku kama wanafanya ibada,” amesema.
Amesema panapokuwepo na viashiria vya kukosekana kwa usalama wa nchi, hicho ndiyo kipaumbele, hivyo lazima washughulikie kwanza jambo hilo.
“Sisi kama Serikali hatuna ugomvi na vyama vya siasa, hata mimi nina chama changu, na vyama vya siasa vipo kikatiba, wala watu wasichanganye haya mambo. Lakini tuna jambo ambalo tuna wajibu nalo, la kuhakikisha Tanzania iko salama na hilo ni jambo la kipaumbele.
“Tumeambiwa kuna watu wanafanya hivi na hivi, tumefuatilia tukajiridhisha, wapo maadui wa taifa letu wanafanya michezo ya aina hiyo, wanataka kuwatumia vijana wa Kitanzania kwa masilahi yao binafsi,” amesema.
Ameongeza: “Kama Serikali ambayo tuna wajibu wa kulinda nchi yetu, wajibu wa kulinda masilahi ya Watanzania, wajibu wa kulinda rasilimali za Watanzania, hatuwezi kupuuza jambo la aina hii.”
Waziri Mkuu amesema kuna wengine wamewakamata ambao wanalipwa, wanataka wawaandikishe vijana wa Kitanzania, wawapeleke barabarani na wameleta watu wa kuwapiga vijana, ili baadaye waichafue nchi, mambo ambayo amesema hawawezi kuruhusu.
“Kuna kijana mmoja wilaya moja, kila mwezi analipwa Sh3 milioni kwa ajili ya kusajili na kushawishi vijana waingie barabarani. Anafanya hayo yote, wale wanaomlipa wana faida gani na nchi yetu? Wanataka wanufaikaje na hayo wanayofapanga?”
“Haya mambo lazima tuambizane ukweli, kuna watu wana nia mbaya na nchi yetu. Mwingine analipwa Sh5 milioni, na tulipomuuliza ametoa siri nyingi, anatumwa na wale waliomtuma, tunajua waliko pia. Na wale wanaomtuma wanalipwa kwa ajili ya shughuli hii,” amesema.
Amesema kila siku watu hao wamekuwa wakipanga siku zenye matukio ya kukusanya watu ili kutekeleza mambo yao na baadaye Serikali ipewe lawama na kuichafua nchi, jambo ambalo amewataka Watanzania kulikataa.
“Hatutacheka na mtu wa namna hiyo. Hatutafanya mchezo na mtu wa aina hiyo, wala tusidanganyane. Tumepewa jukumu la kuilinda nchi hii na watu wake. Huu siyo mtihani wa kwanza, walikuja kutufanyia fujo kule Kibiti nikiwa Waziri wa Mambo ya Ndani,” amesema.
Amesisitiza kwamba mikutano ya vyama vya siasa si jambo linalowashughulisha, bali ulinzi na usalama wa Taifa kwa kuwa hata wao wanataka hao wanaofanya mikutano ya hadhara, pia wawe salama.
“Hatuna mzozo na vyama vya siasa lakini tuna kipaumbele ambacho ni usalama wa Watanzania na tuna taarifa za uhakika ambazo tumeshazifanyia kazi, za watu wanaofanya kazi ya kuratibu uchafuzi wa amani ya Tanzania,” amesema.
Amewataka Watanzania waendelee kufanya kazi zao kwa amani kwani vyombo vya ulinzi na usalama vinashughulikia jambo hilo.
Dk Mwigulu amesisitiza kwamba wanaharakati hawajawahi kuwa na jema na nchi hii, kwani katika awamu mbalimbali walikuwepo na hawajawahi kukoma kwa vitendo vyao vya kuichafua nchi hii na kuhatarisha amani.
Katambi afafanua ukomo
Katika mahojiano yake na BBC Swahili, Waziri Katambi amesema zuio hilo limetolewa kwa sababu za msingi za kiusalama ikiwemo viasharia, dalili na uthibitisho walioupata.
“Hadi pale tutakapoona hali imekuwa salama basi tutaruhusu ili shughuli nyingine za uchumi, kijamii na zile zilizopo kwa mujibu wa sheria lazima ziendelee.
“Kwa kipindi hiki ambacho kuna tishio la kiusalama lazima tuweke nguvu kubwa ya kulinda raia na mali zao.Tutakapojiridhisha kwamba matishio kwa uthibitisho tuliona nao, tutaachia na kuendelea na utaratibu wa kawaida,” amesema Katambi.
Waziri Katambi amesema Watanzania watakuwa mashahidi kwa kile kilichotokea Oktoba 29, 2025 na kusababisha vifo vya Watanzania, uharibifu wa mali za umma na binafsi, huku wananchi wakishindwa kwenda katika majukumu yao.
“Moja ya lawama nyingi ilikuwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwamba vilishindwa kuchukua hatua mapema, kwa viasharia hivyo, sasa tumeona tusidharau taarifa yoyote,” amesema Katambi.
Kwa mujibu wa Katambi, Serikali inachukua hatua za mapema kuepuka machafuko ya athari ka binadamu na kiuchumi, ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.
Na baadaye jana akizungumza na Baraza la Ushauri la Wazee la Manispaa ya Shinyanga, Katambi alisema kwa kuweka zuio la mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa hajavunja Katiba.
Badala yake alisema amefanya hivyo kwa sababu hayuko tayari kuona Taifa linaangamia kwa kuacha kundi la watu wachache wenye masilahi binafsi linakiuka haki za wananchi wengi.
” Kama ni cheo bora kiende, nimesepa hapana, sitakubali kuiacha Tanzania ikiwa kwenye damu, kama ni maisha yangu nipo tayari yapotee, lakini Tanzania ibaki salama,” alisema.
Chadema kujifungia
Wakati huohuo, kamati kuu ya Chadema itajifungia katika kikao kwa siku nne kulijadili jambo hilo kwa kina na kutoa msimamo.
Uamuzi huo umetangazwa leo Juni 27, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche alipozungumza na Mwananchi.
Mwananchi linafahamu kuwa kikao hicho kinatarajiwa kuanza kesho Jumapili Juni 28 hadi Juni 30, kikitanguliwa na kikao cha sekretarieti vitakavyofanyika mkoani Kigoma.
Katika vikao hivyo, Chadema itajidili mwenendo wa hali ya kisiasa, ikiwemo mwenendo wa kesi inayomkabili Tundu Lissu (Mwenyekiti- Chadema), tathimini ya operesheni ya Katiba Mpya, ‘Free Tundu Lissu’ na kupanga ratiba ya mikutano inayofuata.
“Hili jambo si la Heche wala Chadema, bali vyama vya siasa na Watanzania, leo ni kwenye siasa kesho watavunjia sheria katika eneo jingine.
“Narudia hoja ya kuvunja sheria si ya Heche wala Chadema, bali Watanzania, hii si sawa mtu kuvunja sheria na hatuwezi kukubali. Mikutano ya hadhara ipo kisheria, si sawa mtu mmoja kuamka na kuvunja sheria,” amesema Heche.
Kwa mujibu wa Heche, Sheria ya Vyama vya Siasa hairuhusu waziri kuzuia mikutano ya hadhara, akihoji Katambi anapata wapi mamlaka ya kutoa zuio hilo.
Heche amesema hatua ya kuzuia mikutano ya hadhara inalenga kufunga midomo ili watu wasiendelee kuikosoa Serikali na kuwanyamazisha wananchi wasijengewe uwezo kupitia mikutano hiyo.
ACT kutinga mahakamani
Katika kuonyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Serikali wa kuweka zuio la muda mikutano ya hadhara, ACT Wazalendo inajiandaa kupinga hatua hiyo mahakamani.
“ACT Wazalendo tunalaani na kupinga maelekezo hayo haramu kwa nguvu zote na kutoa wito kwa wadau wote kuungana kuzuia jaribio hili na kulinda demokrasia ya nchi yetu.
“Mikutano ya hadhara ni takwa la kikatiba na sheria na si hisani ya waziri na vyombo vya dola,” amesema Rashid Habib Ali, Waziri Kivuli wa Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Ndani wa ACT Wazalendo.
Amesema kwa sasa wanasuribiri kukamilika kwa taratibu mbalimbali ndani ya chama hicho, kisha watatoa taarifa kwa umma kuhusu hatua inayofuata kuhusu suala hilo.
CCM yaahirisha sherehe
Wakati huohuo, Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imetangaza kuahirisha sherehe za Wiki ya Wazazi 2026 zilizokuwa zifanyike Julai 4, 2026 jijini Mwanza, hadi itakapotoa taarifa nyingine.
Uamuzi huo umetangazwa leo Jumamosi, Juni 27, 2026 na Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya hiyo, Fadhili Maganya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Maganya amesema tarehe mpya ya sherehe hizo itatangazwa baadaye baada ya hali kuruhusu.
Maganya amesema sherehe hizo zilikuwa zifanyike kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM na maandalizi yalikuwa yamekamilika huku taarifa zikiwa tayari zimeshawafikia wanachama, viongozi na wananchi.
“Tunapenda kutumia fursa hii kuwataarifu wanachama wetu, viongozi na wananchi wote, hususan wa Jiji la Mwanza, kwamba sherehe hizi zimeahirishwa hadi hapo tutakapowaarifu tena,” amesema Maganya.
Alichokisema Dk Bagonza
Wakati huohuo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amezungumzia zuio hilo akihoji sababu za tamko hilo kutolewa bungeni.
“Zuio la mikutano likatolewa bungeni, tuseme ni Bunge limezuia mikutano? Limetamkwa na waziri, tuseme ni waziri kazuia?
“Kwa nini waziri hakusubiri waziri mkuu ndiye atoe zuio hilo kwa niaba ya Serikali wakati anaahirisha Bunge? Kwa upole hivi mikutano ya kisiasa ni haki ya kikatiba au ni fadhila za Serikali kwa wananchi,” amehoji Dk Bagonza kupitia ukurasa wake wa Facebook.