Dar es Salaam. Licha ya ukuaji wa kasi wa teknolojia duniani, ripoti za hivi karibuni, ikiwemo ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), zinaonyesha wasichana na wanawake bado wako nyuma katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Inaelezwa kwamba hali hiyo ndiyo inayochochea pengo la kijinsia katika uchumi wa kidijitali. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2024 ijulikanayo kama ‘Technology on Her Terms,’ wanawake milioni 244 duniani hawatumii intaneti ikilinganishwa na wanaume, jambo linalowanyima fursa muhimu za elimu, ajira na ubunifu katika ulimwengu wa kidijitali.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, pengo la ujuzi wa kidijitali ni kubwa zaidi, ambapo kwa kila wanaume 100 wenye uwezo wa kutumia programu za kompyuta kama spreadsheet, wanawake kati ya 40 hadi 44 tu ndiyo wana ujuzi huo.

Aidha, wanawake wanawakilisha takribani asilimia 35 pekee ya wahitimu wa masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) duniani, huku ushiriki wao katika tafiti za sayansi na teknolojia ukiwa karibu asilimia 29 tu.

Ripoti ya mwaka 2025 ya shirika la International Telecommunication Union (ITU), “Facts and Figures 2025,” inaonyesha uwiano wa usawa wa kijinsia katika matumizi ya intaneti duniani ni 0.92, ukimaanisha wanawake bado wako nyuma ya wanaume.

Pia, hakuna maendeleo makubwa tangu mwaka 2019 katika kuondoa pengo hili la kidijitali, ambapo Afrika bado iko nyuma zaidi, licha ya maboresho kidogo katika miaka ya karibuni. Kwa lugha rahisi, wanaume bado wana uwezekano mkubwa zaidi wa kutumia intaneti kuliko wanawake duniani.

Ripoti nyingine ya World Economic Forum (Global Gender Gap Report 2025) inaonyesha usawa wa kijinsia duniani bado uko mbali kufikiwa na unaweza kuchukua zaidi ya miaka 100 kufikia usawa kamili.

Ripoti hizi zote zina ujumbe mmoja kwamba pengo la kijinsia katika Tehama bado ni kubwa na linajitokeza katika upatikanaji wa intaneti, ujuzi wa kidijitali na ajira za teknolojia.

Bila hatua za makusudi, pengo hili linaweza kuendelea kwa muda mrefu. Kwa ujumla, tafiti hizo za ITU na World Economic Forum zinaunga mkono yale yanayosemwa na Unesco kwamba, licha ya maendeleo ya teknolojia duniani, wasichana na wanawake bado hawashiriki kikamilifu katika Tehama.

Ripoti hizi zinatolewa wakati dunia leo, Alhamisi, Aprili 23, 2026, ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Tehama inayolenga kuhamasisha ushiriki wa wasichana katika sekta ya teknolojia na kupunguza pengo la kijinsia lililopo.

Wataalamu wanasema hali hiyo inachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwamo mitazamo ya kijamii inayodhoofisha nafasi ya wasichana katika teknolojia, ukosefu wa vifaa na miundombinu ya kidijitali, pamoja na changamoto za usalama mtandaoni.

Mchumi aliyejikita katika uchumi wa kidijitali, Francis Nyonzo, anasema msingi wa Tehama ni sayansi inayoanzia ngazi ya msingi.

“Inahitaji msingi mzuri wa hesabu. Pili, suala zima la teknolojia, wanawake wanaonekana kama watumiaji (consumers) badala ya kuonekana kuwa watu wanaoweza kutengeneza vitu,” amesema Nyonzo wakati akizungumza leo na Mwananchi kwa simu.

Nyonzo amesema kwa Tanzania usawa upo kuanzia sera na uhamasishaji wa ushiriki wa wanawake katika sayansi, ila bado kuna nguvu inahitajika katika utekelezaji wa vitendo.

Changamoto nyingine zinazotajwa ni mitazamo ya kijamii ambapo teknolojia huonekana kama taaluma ya wanaume, na upatikanaji mdogo wa vifaa na mtandao kwa wasichana, hasa katika maeneo ya vijijini.

Aidha, ukosefu wa mifano ya kuigwa katika sekta ya teknolojia pamoja na changamoto katika masuala ya usalama mtandaoni huwakatisha tamaa baadhi ya wasichana kushiriki kikamilifu.

Unesco inapendekeza kuimarishwa kwa elimu ya kidijitali shuleni, kuondoa vikwazo vya kijinsia vinavyowazuia wasichana kuingia katika sekta ya teknolojia, kuhamasisha elimu ya kidijitali kwa wasichana kupitia miradi maalum, kuongeza mafunzo ya STEM, kukuza programu za ulezi na kupinga ubaguzi wa kijinsia katika teknolojia.

Unesco inaonyesha kuwa, ingawa maendeleo yanaonekana, bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha wasichana wanapata fursa sawa katika Tehama.

Kuwawezesha wasichana katika teknolojia si tu suala la usawa, bali pia ni muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na ubunifu wa jamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *