Miongoni mwa waliopata fursa hiyo adimu kupitia mchakato wa bahati nasibu ni Irene Kitoti kutoka Tanzania, mwanaharakati kijana wa haki za watoto ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa asasi ya Genesis for Children Organization aliyebeba sauti ya vijana wa Tanzania kwenye jukwaa hilo la kimataifa.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema “Nilifurahi sana kuchaguliwa. Maswali yangu ndiyo yalinipa nafasi hii,” anasema, akielezea safari yake ya kufika katika mazungumzo hayo muhimu ya mchakato wa kumpata Ktibu Mkuu mpya  anayetarajiwa kushika hatamu kuanzia Januari Mosi 2027.

Picha ya mwanamke mweusi mwenye tabasamu akiwa amevaa shuka la rangi ya kijani, bluu, na manjano ambalo linaandikwa juu yake 'TANZANIA'. Amevaa suti na amesimama mbele ya tapestry kubwa.

UN News/Feissal Kirwa

Irene Kitoti (Kushoto) kutoka Tanzania, Mwanaharakati kijana wa haki za watoto ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa asasi ya Genesis for Children Organization akihojiwa na Flora Nducha wa UN News Kiswahili.

Kutafuta fursa, si kusubiri

Kwa Irene, kushiriki katika mchakato huo hakukuwa bahati bali matokeo ya juhudi binafsi na kujituma.

Akiwa mwanachama wa mifumo mbalimbali ya vijana ndani ya Umoja wa Mataifa, aliamua kuchukua hatua na kuomba nafasi hiyo.

“Mimi ni mtu ambaye napenda kutafuta fursa. Sikungoja kuitwa nilijitokeza mwenyewe nikafanya usajili,” anasisitiza.

Kupitia ushiriki wake katika mitandao ya vijana na mawasiliano ya kidijitali ya Umoja wa Mataifa, Irene alifanikiwa kuchaguliwa si tu kama mshiriki bali pia kama mzungumzaji na mwangalizi wa mchakato huo.

Maswali mazito kuhusu mustakabali wa watoto

Katika mjadala huo, Irene aliweka mezani maswali magumu yanayogusa kiini cha changamoto za dunia hasa kwa watoto katika maeneo ya migogoro.

“Je, watawalinda vipi watoto katika maeneo yenye vita na kuhakikisha uwajibikaji kwa wanaokiuka haki zao?” alihoji.

Swali lake la pili lililenga janga la watoto kupoteza maisha katika migogoro na ukosefu wa elimu,

“Watoto wengi wasio na hatia wanakufa kila siku. Je, kama Katibu Mkuu, utafanya nini kuhakikisha wanapata haki ya kuishi na kupata elimu?”

Amesisitiza kuwa elimu ni haki ya msingi na kwamba vita na siasa haziwezi kuendelea kuwanyima watoto na vijana hakiya mustakabali wao.

Wito kwa viongozi: Weka dunia mbele

Akizungumza kuhusu matarajio yake kwa Katibu Mkuu ajaye wa Umoja wa Mataifa, Irene ametoa wito kwa nchi wanachama kuchagua kiongozi anayejali maslahi ya dunia nzima badala ya maslahi binafsi au ya taifa lake.

“Tunataka kiongozi anayesikiliza watu na kuweka maslahi ya wote mbelena sio siasa binafsi,” anasema.

Ameongeza kuwa kiongozi huyo lazima awe karibu na wananchi, hasa vijana, na awe tayari kushirikiana nao katika kutafuta suluhu za changamoto za kimataifa.

Vijana wajitokeze na kushiriki

Kwa vijana wenzake, Irene ana ujumbe mmoja ulio wazi, usisubiri fursa ikufuate nenda uitafute.

“Hakuna atakayejua unahitaji nini kama hautajitokeza. Tafuta fursa, jitolee na ujielimishe,” anasema.

Anasisitiza umuhimu wa kaziza kujitolea kama njia ya kujenga uzoefu na mtandao wa kimataifa, akieleza kuwa mafanikio yake yametokana na uwajibikaji na ushirikiano na wengine.

Ndoto ya kizazi kipya katika jukwaa la kimataifa

Safari ya Irene Kitoti inaakisi nguvu ya vijana katika kuunda mwelekeo wa maamuzi ya kimataifa. Kupitia sauti yake, masuala ya watoto, elimu na haki za binadamu yamepata nafasi katika mjadala wa juu kabisa wa uongozi wa dunia.

“Vijana tuna nafasi. Tukijitokeza, tunaweza kuibadilisha dunia,” anasema kwa kujiamini.

Katika ulimwengu unaokabiliwa na migogoro na changamoto nyingi, sauti kama ya Irene zinaonesha kuwa matumaini ya kesho yapo mikononi mwa kizazi kinachothubutu kuzungumza leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *