Katika uamuzi uliotolewa hii leo, mahakama imeeleza kuwa kuna msingi wa kutosha kuamini kuwa Duterte anawajibika kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji na majaribio ya mauaji chini ya Kifungu cha 7(1)(a) cha mkataba wa Rome (Mkataba wa kuanzishwa kwa ICC)

Mashtaka yahusishwa na kampeni ya “vita dhidi ya dawa za kulevya”

Majaji hao wa Chumba cha Awali walibaini kuwa makosa hayo yalifanyika kati ya mwezi Novemba 1, 2011 na Machi 16, 2019, katika muktadha wa kampeni ya “vita dhidi ya dawa za kulevya” iliyotekelezwa nchini Ufilipino.

Kwa mujibu wa uamuzi huo, mashambulizi hayo yalikuwa ya “kuenea na ya kimfumo” dhidi ya raia, jambo linalokidhi vigezo vya uhalifu dhidi ya ubinadamu chini ya sheria za kimataifa.

Ushahidi wa pande zote wazingatiwa

Mahakama ilisema imefikia hitimisho hilo baada ya kupitia ushahidi na hoja zilizowasilishwa na upande wa mashtaka pamoja na utetezi wakati wa kikao cha kuthibitisha mashtaka kilichofanyika kati ya tarehe 23 na 27 Februari 2026.

Vilevile, mahakama ilizingatia nyaraka na mawasilisho ya waathirika walioshiriki katika mchakato huo kupitia wawakilishi wao wa kisheria.

Hatua inayofuata

Kesi sasa itahamishiwa kwenye chumba cha kusikiliza kesi, ambacho kitaamua ratiba na hatua zinazofuata za mwenendo wa kesi.

ICC imesisitiza kuwa kesi zake hufanyika kwa haki na bila upendeleo, huku ikihakikisha upande wa utetezi unapata muda wa kutosha kujiandaa, pamoja na kulinda haki za waathiriwa.

Historia ya kesi

Hati ya kukamatwa kwa Duterte ilitolewa kwa siri tarehe 7 Machi 2025 na baadaye kuwekwa wazi tarehe 11 Machi 2025. Alikabidhiwa rasmi kwa ICC tarehe 12 Machi 2025 na kufikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 14 Machi 2025.

Kikao cha kuthibitisha mashtaka kilifanyika Februari 2026 mbele ya jopo la majaji lililoongozwa na Iulia Antoanella Motoc, likishirikisha pia Reine Adélaïde Sophie Alapini-Gansou na María del Socorro Flores Liera.

Soma zaidi kuhusu kesi hiyo hapa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *