Wakati wa ziara ya kiserikali ya Rais wa Chad Mahamat Idriss Déby huko Algiers, nchi hizo mbili zimesaini mikataba kadhaa, hasa katika sekta ya uchumi. Jambo muhimu zaidi kuhusu sekta ya hidrokaboni, ikiwa ni pamoja na kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ambapo kampuni ya Algeria ya Sonatrach ltasaidia Chad katika kujenga kiwanda cha kusafishia mafuta chenye uwezo wa kuzalisha hadi mapipa 20,000 ya mafuta kwa siku.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Katika siku ya pili ya ziara yake ya kiserikali nchini Algeria, Rais wa Chad Mahamat Idriss Déby alikutana ana kwa ana na mwenzake wa Algeria, Abdelmadjid Tebboune, ambaye alimkaribisha kwa dhati, kabla ya kuongoza sherehe ya kusaini mikataba ya pande mbili zaidi ya thelathini – mikataba 34, kulingana na ofisi ya rais wa Chad.

Mikataba mitatu muhimu zaidi inahusu sekta ya hidrokaboni, hasa kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano kati ya kampuni ya Algeria ya Sonatrach na kampuni ya Hidrokaboni ya Chad (SHT) kwa ajili ya kuundwa kwa kiwanda cha kusafishia mafuta chenye uwezo wa kuzalisha hadi mapipa 20,000 kwa siku. Mkataba huu unakuja wakati ambapo N’Djamena “iko katika hatua ya kujaribu kutofautisha uwezo wake wa uzalishaji. Nchi hii inatafuta kuvutia wawekezaji wapya ili kuendeleza maliasili zake, hasa katika sekta ya mafuta,” anaelezea mwanauchumi wa Chad Djimadoum Mendekor. “Kwa nchi hii isiyo na ajira na viwanda, ni muhimu kuongeza idadi ya makampuni yatakayokuja kufanya kazi nchini humo,” anaongeza.

Katika upande wa nishati, makubaliano ya mfumo kati ya N’Djamena na kampuni ya Petroli ya Algeria pia yalianzishwa ili kuimarisha na kuongeza uwezo wa sekta ya mafuta ya Chad, huku mikataba mingine ikifungua njia ya kuanzishwa kwa viwanda vya Algeria nchini Chad katika sekta za viwanda, madini, na nishati mbadala.

“Kuipiku Morocco”

Kwa upande mwingine, makubaliano hayo yanahusu sekta mbalimbali, kuanzia mawasiliano na kazi za umma hadi afya ya wanyama, usafiri wa anga, na elimu ya juu. Usalama, kwa upande wake, ulikuwa mada ya makubaliano ya ushirikiano kati ya mawaziri katika mapambano dhidi ya ugaidi.

Wakati Mahamat Idriss Déby akiwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa sherehe kwamba ziara yake ilionyesha “nia ya wazi ya kisiasa kwa upande wa nchi zote mbili ya kuhama kutoka urafiki wa jadi hadi ushirikiano wa kimkakati wa kizazi kipya,” Algeria inaona mfululizo huu wa kihistoria wa makubaliano kama uthibitisho wa msimamo wake barani Afrika.

Kwa kuwa tayari imesaini makubaliano kadhaa na Niger kufuatia ziara ya Rais Abdourahamane Tiani huko Algiers mnamo mwezi Februari mwaka huu, Algeria inarudi kwa nguvu barani Afrika kwa lengo la “kuipiku Morocco, kutokana na ushindani mkubwa kati ya nchi hizo mbili katika Kusini mwa Jangwa la Sahara,” ambapo zote zinatafuta kupanua ushawishi wao, anaelezea Michaël Ayari, mchambuzi wa Algeria na Tunisia kutoka Shirika la Kimataifa linalotatua migogoro International Crisis Group (ICG.

Rabat na N’Djamena pia hivi karibuni ziliamua kushirikiana, huku, kwa upande mmoja, kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji ya Morocco nchini Chad—hasa katika sekta za nishati na utamaduni—na kwa upande mwingine, uzinduzi wa ubalozi mdogo wa Chad huko Dakhla, Sahara Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *