
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi katika nafasi mbalimbali za Serikali, hatua inayolenga kuimarisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika taasisi za umma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, uteuzi huo unaanza kutekelezwa mara moja, huku viongozi walioteuliwa wakitarajiwa kuanza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu za utumishi wa umma.
Walioteuliwa ni mbunge Angela Kizigha ambaye anakuwa Mshauri wa Rais, Masuala ya Jamii.
Uteuzi huo unakuja ikiwa ni mwendelezo wa imani kubwa aliyopewa na Rais Samia, baada ya hapo awali Aprili 2, 2025 kuteuliwa kuwa Mbunge wa kuteuliwa kupitia nafasi 10 za Rais.
Katika uteuzi mwingine, Peter Mwasalyanda ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), akichukua nafasi ya Dk Jabiri Bakari aliyemaliza muda wake.
Kabla ya uteuzi huo, Mwasalyanda alikuwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo alisimamia miradi ya kupanua huduma za mawasiliano hususan maeneo ya vijijini na yasiyofikiwa kwa urahisi.
Kwa upande mwingine, Dk Jabiri Bakari ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), akichukua nafasi ya Salim Msangi ambaye amepangiwa majukumu mengine serikalini.
Aidha, Balozi Mobhare Matinyi ameteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Algeria, uteuzi umelenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na taifa hilo la Afrika Kaskazini.
Matinyi ni mwanadiplomasia na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya mawasiliano ya umma na diplomasia.
Kabla ya uteuzi huu, aliwahi kulitumikia Taifa kama Balozi wa Tanzania nchini Sweden, ambapo alijikita katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi, elimu na uwekezaji kati ya Tanzania na nchi za Ulaya.