
Chunya. Mkazi wa Kata ya Chokaa, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Almas Ramadhani (35), amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kufanya shambulio la aibu dhidi ya mtoto wa miaka mitatu kwa kumshika sehemu zake za siri.
Hukumu hiyo ilisomwa Juni 23, 2026 na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, James Mhanuzi, baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka bila kuacha shaka yoyote.
Akisoma maelezo ya kesi hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Pastory Machupa, alidai kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Mei 25, 2026 katika Kijiji cha Mlimanjiwa, Wilaya ya Chunya.
Mahakama ilielezwa kuwa siku ya tukio mshtakiwa alimkuta mtoto huyo akicheza na wenzake, kisha alimshika mkono na kumpeleka nyuma ya nyumba ambako alianza kumshika sehemu zake za siri.
Machupa alidai kuwa wakati mshtakiwa akiendelea na kitendo hicho, mmoja wa majirani alimwona kupitia dirishani na kutoa taarifa kwa majirani wengine, ambao walifika eneo la tukio na kufanikiwa kumkamata.
Kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, upande wa mashtaka uliomba adhabu kali itolewe ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia za ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
Ombi hilo liliungwa mkono na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Mwajabu Tengeneza, ambaye alisisitiza umuhimu wa mahakama kutoa adhabu kali ili kusaidia kukomesha vitendo vya udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto.
Baada ya kupitia ushahidi wote ulio wasilishwa, Hakimu Mhanuzi alimtia hatiani mshtakiwa na kumhukumu kutumikia kifungo cha miaka 20 jela.
Hakimu huyo pia alieleza kuwa mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa endapo hajaridhika na hukumu iliyotolewa.
Wakati huohuo, Mahakama ya Wilaya ya Chunya imemhukumu Charles Semu (28) kifungo cha miaka 20 jela baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki vipande viwili vya ngozi ya mnyama pori aina ya nyati bila kibali.
Hukumu hiyo pia ilisomwa Juni 23, 2026 na Hakimu Mhanuzi baada ya mahakama kuridhishwa na ushahidi uliotolewa dhidi ya mshtakiwa.
Mahakama ilielezwa kuwa Semu alitenda kosa hilo Februari 18, 2026 katika Pori la Akiba la Lukwati-Piti, lililopo Kijiji cha Bintimanyanga, Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.