Dar es Salaam. Pendekezo la kupatikana kwa Katiba mpya ifikapo 2028, limefungua mjadala upya wa kitaifa kwa vyama vya siasa, viongozi wa dini na wananchi, wakisema ikiwa litafanikiwa litakwenda kuzalisha Tanzania mpya.
Kwa nyakati tofauti, wakizungumza na Mwananchi siku moja baada ya pendekezo hilo kutolewa, wadau hao wamesema kupatikana kwa Katiba mpya ni matamanio ya muda mrefu ya Watanzania walio wengi.
Hata hivyo, wametoa angalizo mchakato mpya utakapoanza, masuala muhimu yanayolalamikiwa kwa muda mrefu yapewe umuhimu.
Pendekezo la kupatikana kwa Katiba mpya ifikapo 2028 ni miongoni mwa yaliyotolewa kwenye ripoti ya Jaji Othman Chande iliyowasilishwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026, kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025, Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othman akisoma Muhtasari wa Ripoti ya Tume hiyo, Ikulu jijini Dar es Salaam, Aprili 23, 2026.
Akiwasilisha taarifa hiyo, pamoja na mambo mengine, mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Chande alipendekeza kupatikana kwa Katiba mpya ifikapo 2028 ambayo itatumika kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2029 na Uchaguzi Mkuu wa 2030.
“Ili kufikia lengo la kupata Katiba kabla ya 2029, Serikali iunde Kamati ya Wataalamu wa Katiba ambayo itakuwa na jukumu la kupitia Katiba iliyopo, rasimu ya Katiba ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Pendekezwa ya Mwaka 2014, ripoti za Tume, Kamati na Vikosi Kazi mbalimbali. Baada ya kufanya mapitio ya nyaraka hizo, Kamati ya Wataalamu itapata maoni na michango ya wananchi na kisha kuandaa rasimu ya Katiba mpya itakayopigiwa kura na wananchi,” alisema Jaji Chande.
Pendekezo hilo limepokewa kwa mitazamo tofauti na vyama vya siasa, viongozi wa dini na baadhi ya wanachi.
Kwa nyakati tofauti wakizungumza na Mwananchi, wamesema Katiba mpya ni hitaji la Watanzania wengi, kama litafanikiwa basi litakwenda kuzalisha Tanzania mpya.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu amesema Katiba mpya ilitakiwa ipatikane tangu huko nyuma, akisisitiza kwamba pendekezo la Jaji Chande ifikapo 2028 iwe imepatikana lichukuliwe kwa uzito.
Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu
“Hata mchakato utakapoanza usiwe wa ni zoezi la bora liende, liwe na matokeo ya ushirikishwaji wa wananchi, masuala muhimu yaliyolalamikiwa kwa muda mrefu yapewe umuhimu katika mchakato wote,” amesema Semu.
Amesema matamanio ya ACT ni mchakato wake uwe na dhamira itakayobeba maono na matamanio ya Watanzania ya kujenga taifa la haki linalosimamia demokrasia na kujenga maendeleo ya pamoja.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu naye amesema hitaji la Katiba mpya ni la muda mrefu na mara kwa mara presha ya upatikanaji wake inakuwa kubwa kutokana na mazingira.
Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu
Amesema kupatikana kwake kunaweza kuzalisha Tanzania mpya na Watanzania wote kuanza safari wakiwa wamoja.
Ameshauri mchakato ukianza mifumo yote ya haki izingatiwe, iweke uimara wa mihimili ya Bunge, Mahakama na Serikali sanjari na mhimili usio rasmi wa habari ili kila kimoja kitimize wajibu wake ipasavyo.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Makamu mwenyekiti wake John Heche amesema suala hilo watalitolea maoni na msimamo wa chama baada ya kamati kuu kukaa Aprili 29.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche
“Tutaichambua kwa kina ripoti, ikiwamo hilo pendekezo la Katiba mpya,” amesema Heche alipozungumza na Mwananchi leo Aprili 24, 2026.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Joseph Selasini amesema Jaji Chande ametoa pendekezo, lakini bado wana wasiwasi na utekelezaji wake, japokuwa kama litafanikiwa, basi litaleta mwanga mpya.
Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini
‘Hili pendekezo la Jaji Chande lisiishie tu kutamka, lifanyiwe utekelezaji isionekane kama Katiba mpya inatolewa kwa hisani. Wananchi tulio wengi tunaotawaliwa ndiyo tunaitaka, ikiwepo inaweza kubadilisha maisha ya wananchi kama itapatikana kwa ridhaa yao,” amesema.
Aliyekuwa mgombea Mwenza wa Chama cha Wananchi (CUF) kwenye uchaguzi mkuu wa 2025, Husna Abdallah amesema Katiba mpya ikipatikana itasaidia kupunguza migogoro ya kisiasa kwa kiwango kikubwa.
Kilio cha Watanzania
Akitoa maoni kuhusu suala hilo, Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo amesema Katiba mpya ndicho kilio cha Watanzania kwa miaka mingi kabla ya 2025.
“Natamani kuona ndani ya muda pendekezwa tunapata Katiba mpya, moja ya vitu vinavyopaswa kufanyika mapema ni kuanza mchakato huo na maridhiano,” amesema.
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo
Amesema nchi inahitaji kurudi pamoja na kuombana msamaha, akibainisha kwamba mapendekezo ya ripoti ya Jaji Chande ni hatua ya kuelekea huko na kuliponya taifa.
Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Nuhu Mruma amesema ripoti ya Jaji Chande suala hilo wamelipokea kwani yote yanayotakiwa kufanyika ni kutengeneza ustawi wa jamii.
“Nimeisikiliza ripoti ina mapendekezo mazuri, kama viongozi wadini kushirikishwa katika baadhi ya mapendekezo ni jambo zuri, Bakwata tumelipokea kwani nyuma ya dini kuna watu wengi, hivyo ushirikishwaji utasaidia kuwa na mustakabali wa pamoja.
Alipoulizwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa amesema Baraza hilo bado linaichambua ripoti ya Jaji Chande na watatoa maoni yao hivi karibuni.
“Bado tunaichambua ripoti yote na kuichakata ili kutoa maoni yetu kama TEC ikiwamo hilo la Katiba mpya,” amesema Pisa, ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Lindi.
Suluhu migogoro ya kisiasa
Baadhi ya wananchi wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu Katiba mpya, wengine wakiamini kupatikana kwake itakuwa suluhu ya migogoro ya kisasa na wengine wakisema hata ikitungwa iliyo bora zaidi, kama utelekezaji wake hautozingatiwa haitakuwa na maana.
Mkazi wa Morogoro, Seleman Hamidu amesema licha ya umuhimu wa Katiba mpya, hata hiyo iliyopo ni nzuri lakini utekelezaji haupo, akisisitiza Katiba mpya haiwezi kuwa na maana yoyote kama hakuna utekelezaji.
Zebia Nelson wa Dar es Salaam yeye ameshauri ukianza mchakato wa Katiba mpya, baadhi ya mambo yaboreshwe akishauri pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) apewe meno, badala ya kuishia kuwasilisha ripoti tu ya ubadhirifu.
James Paulo wa mkazi wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara, amesema utelekezaji wa Katiba mpya utategemea watu watakaopewa hiyo dhamana na uwajibikaji wake.
Ameshauri kuwepo tume huru ya uchaguzi ambayo itazalisha watu sahihi ambao ni machaguo ya wananchi watakaowajibika kwa wananchi pale wanapokwenda kinyume.