Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini China, Khatibu Makenga, amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi umeendelea kuimarika katika kukuza biashara na diplomasia ya uchumi kwa Watanzania wanaoishi nchini humo.
Akizungumza katika kongamano la biashara jijini Guangzhou, Makenga ambaye amemuwakilisha mgeni rasmi, amesema katika kipindi cha miaka minne aliyofanya kazi eneo la Guangdong, ameshuhudia maendeleo makubwa ya biashara na mchango wa diaspora katika uchumi.
Ameeleza kuwa Diaspora of Tanzanians in China (DITAC) imekuwa chachu muhimu ya kukuza diplomasia ya uchumi kwa kushirikiana kwa karibu na ofisi ya Konseli Kuu ya Tanzania, inayosimamia majimbo kadhaa ikiwemo Fujian, Hainan, Guangxi, Jiangxi na Hunan.
Aidha, Makenga amepongeza mchango wa taasisi za kifedha za Tanzania, zikiwemo CRDB Bank, NBC Bank Tanzania na NMB Bank, akisema zimekuwa kichocheo muhimu kwa kutoa mitaji na ushauri kwa wafanyabiashara na wajasiriamali waliopo China.
Amesisitiza kuwa mazingira ya amani na utulivu pamoja na utekelezaji wa sera za mambo ya nje za Tanzania vimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya shughuli za biashara kwa diaspora.
Kwa upande mwingine, amesema kampuni na wafanyabiashara wa Kitanzania waliopo China wamekuwa wakibuni mbinu za kibiashara zikiwemo kaulimbiu za kuvutia wateja, hatua inayosaidia kuongeza imani na ufanisi katika biashara za usafirishaji na usambazaji wa bidhaa kati ya China na Tanzania.
Makenga amehitimisha kwa kupongeza wadau wote wanaochangia kukuza biashara na uwekezaji, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano huo kwa manufaa ya uchumi wa taifa.
(Feed generated with FetchRSS)