
Wachimbaji madini zaidi ya mia moja kutoka kampuni ya Doruk Madencilik wamekuwa wkiandamana mbele ya Hifadhi ya Kurtulus katikati mwa Ankara kwa siku kadhaa. Wachimbaji hao madiniambao wanatokea katika jiji la Eskişehir, umbali wa takriban kilomita 200, wanadai usaidizi kutoka Wizara ya Nishati na Maliasili ili kupata malipo ya mishahara ambayo haijalipwa kwa miezi kadhaa. Baada ya kukataliwa kukutana na mamlaka, walianza mgomo wa kula siku Jumatatu, Aprili 20.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu huko Ankara, Céline Pierre-Magnani
Vikosi vya usalama vilijaribu kuwatawanya wachimbaji madini hao waliokuwa wanapiga kambi katika Hifadhi ya Kurtulus Nchini Ankara kwa kurusha mabomu ya kutoa machozi. Wakiwa wameketi chini, bila shati, wakiwa na chupa za maji mikononi, wachimbaji hao madini walitenganishwa na umati wa watu kwa kamba iliyowekwa na polisi. Wamechagua kubaki kimya wakati wa mgomo wao wa kula, lakini mara kwa mara hupiga kofia zao ngumu za njano ardhini kuelezea kupinga kwao.
Wakili wao, Abdurrahim Demiryürek, anaelezea kwamba amekuwa akijaribu kukutana na mamlaka: “Tunajaribu kupata miadi na Wizara ya Nishati na Wizara ya Kazi, pamoja na viongozi wa kampuni,” anasema. Anaongeza: “Tulikuwa tumezungukwa na polisi mbele ya Wizara ya Nishati. Mara tu tulipofika, tulianza mgomo wa kula. Sasa tuko katika siku yetu ya tano ya mgomo. Tunachodai ni kwamba wachimbaji wote wapokee pesa wanazodai.”
Vyama vya wafanyakazi, kamati za wanafunzi, na umma wamekuja kuonyesha uungaji mkono wao kwa wachimbaji hao madini, ambao wanapanga kuendelea na mgomo wao wa kula hadi madai yao yatimizwe. Wakati huo huo, kampuni ya Doruk Madencilik inatafuta kujadiliana na chama cha wafanyakazi chenye ushirikiano wa karibu na uongozi wa kampuni .
Uturuki ina akiba kubwa ya makaa ya mawe na ni mzalishaji wa tatu kwa ukubwa duniani wa makaa ya mawe ya kahawia au brown coal. Sekta ya madini pia imegubikwa na majanga mabaya, kama vile moto uliozuka katika mgodi wa Soma mwaka wa 2014, ambao uliua watu 301 magharibi mwa nchi.