Marekani. Mtoto wa staa wa Pop na RnB kutokea Marekani, Rihanna (38), Rocki Irish, ameandika historia kwa kutokea ukurasa wa mbele (cover) kwenye jarida akiwa na umri wa miezi sita tu, na ikiwa ni mara yake ya kwanza.
Mwimbaji huyo ameonekana kwenye toleo la Pop Issue la jarida la W Magazine akiwa amembeba mtoto huyo, huku wote wawili wakiwa wamevalia mavazi ya kifahari kutoka chapa ya Dior Haute Couture.
Rihanna alivaa koti jeusi lenye mapambo ya manyoya meupe shingoni pamoja na kofia ya rangi ya zambarau, huku mwonekano wake ukikamilishwa na vipodozi vyenye rangi ya kuvutia pamoja na mkufu wa Cartier.
Naye mtoto Rocki alivaa nepi ya kifahari ya Dior Haute Couture pamoja na mapambo ya maua kichwani, mtindo ambao unafanana na ule wa mama yake.
Rihanna, mkali wa kibao cha Diamonds (2012), inasemekana kuwa ndiye mtu wa kwanza maarufu kuonekana akivaa mapambo hayo yaliyotoka kwenye maonyesho ya mitindo yaliyofanyika Paris, Ufaransa.
Mkurugenzi wa kitengo cha ubunifu kutoka Dior, Jonathan Anderson ambaye alisimamia mavazi ya Rihanna na Rocki, pamoja na kuwabunia pia mavazi watoto wake wengine, RZA na Riot, alieleza kuhusu ubunifu huo.
“Hi ni mara ya kwanza kwa Dior kutengeneza nepi ya Haute Couture,” alisema Jonathan na kuongeza.
“Rihanna anapokuwa na wazo hunishirikisha, mara nyingi huwa yuko mbele ya wakati. Anafikiri nje ya box, na mimi huwa namuamini kabisa katika mipango yake,” alisema.
Upigaji picha wa jalada la jarida hilo ulifanywa na mpiga picha maarufu Tim Walker anayejulikana kwa ubunifu wa kipekee kwa kupiga picha za mitindo, huku mitindo yote ikiratibiwa na Jahleel Weaver.
Kwa ujumla, tukio hilo linaashiria mwanzo wa safari ya Rocki katika tasnia ya mitindo, akifuata nyayo za mama yake ambaye ameendelea kuwa miongoni mwa watu wenye ushawishi mkubwa katika ulimwengu huo.
Utakumbuka kuwa Rocki ndiye mtoto pekee wa kike wa Rihanna kati ya watoto watatu aliyojaliwa katika uhusiano wake na rapa Asap Rocky.
Mtoto wake wa kwanza, RZA alizaliwa Mei 13, 2022, mwaka uliofuatia akajifungb ua mtoto wa pili, Riot hapo Agosti 1, 2023, na wa tatu, Rocki akazaliwa Septemba 13, 2025.
Rocki alipewa jina hilo kama sehemu ya kulipa heshima jina la kisanii la baba yake (Rocky) na ndio sababu yamefanana sana yakipishana tu herufi za mwishoni -’I’ na ‘Y’.
Ikumbukwe jina ‘Asap Rocky’ linatokana na jina lake la utani – Rocky, na la kundi lake lake la Hip Hop, A$AP, ambalo aliwahi kueleza kuwa linamaanisha; Always Strive And Prosper – Daima jitahidi na ufanikiwe.