KOCHA Msaidizi wa Mlandege, Sabri China, amekiri kuvutiwa na kiwango kizuri cha mshambuliaji wa timu hiyo, Mussa Hassan ‘Mbappe’ huku akisema ameona kitu kikubwa kutoka kwake.

Amesema, amestahili kuitwa hivyo kwa sababu ana kila sifa alizonazo mchezaji mwenye jina hilo, Kylian Mbappe anayecheza Real Madrid na timu ya taifa ya Ufaransa. Akitaja sifa hizo ni pamoja na kasi na uwezo wa kutembea na mpira akiwa uwanjani.

“Mussa ni mchezaji mzuri mwenye kiwango kikubwa na akiamua kucheza mpira ana uwezo wa kufika mbali zaidi ya alipo sasa,” amesema China.

Amefafanua, kati ya mambo yanayomfanya kusonga mbele ni namna mchezaji huyo alivyo msikivu na muelewa anapopewa maelekezo.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo amesema anapenda kuzingatia maelekezo ya mwalimu na kutumia mbinu zake kupenya safu ya ulinzi ya washindani kuiandikia matokeo mazuri.

Pia, amesema mashabiki wa timu hiyo wanampa hamasa sana wakiwa uwanjani na anapambana ili kuwapa furaha kadiri anavyoweza.

Amewasisitiza mashabiki wa Mlandege waendelee kufika uwanjani na hawatakiwi kuikatia tamaa kwani imerudi kwenye ubora wake.

Mshambuliaji huyo Aprili 23 mwaka huu, alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 ilioupata Mlandege katika robo fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Singida Black Stars na kufuzu nusu fainali ikienda kucheza dhidi ya Simba, leo Jumapili, michuano inayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Kabla ya hapo, alifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Muembe Makumbi City ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Zanzibar iliyochezwa Apriliu 18, 2026 kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *