
Ushindi wa mechi tatu mfululizo umetajwa kuibua morali mpya ndani ya kikosi cha Tanzania Prisons, huku timu hiyo ikibainisha kuwa mchezo ujao dhidi ya Singida Black Stars utakuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatma yao kwenye Ligi Kuu.
Prisons haikuwa na mwanzo mzuri wa msimu hadi kufikia hatua ya uongozi kubadilisha makocha mara tatu, lakini sasa timu hiyo imeonekana kupata mwanga mpya kutokana na mfululizo wa ushindi katika michezo yao ya hivi karibuni.
Kikosi hicho cha Jeshi la Magereza kilianza kwa ushindi wa mabao 3-2 jijini Mwanza, kisha kikarejea Uwanja wa Sokoine na kuilaza Dodoma Jiji mabao 3-1, na baadaye kuifunga JKT Tanzania bao 1-0. Matokeo hayo yameiwezesha Prisons kupanda hadi nafasi ya 14 kwa pointi 26.
Kwa sasa, timu hiyo inajiandaa na michezo mitatu iliyobaki: ikianza dhidi ya Singida Black Stars Juni 24 mjini Singida, kisha kurejea Mbeya kuikabili Mtibwa Sugar, na kumalizia ugenini dhidi ya Mashujaa.
Nahodha wa timu hiyo, Lambart Sabiyanka, amesema timu kwa sasa ina ari na morali kubwa kutokana na ushindi huo wa mfululizo, akisisitiza kuwa kilichobaki ni kulinda heshima ya Tanzania Prisons.
Alisema ushindi dhidi ya Singida Black Stars unaweza kuwa hatua muhimu ya kuhakikisha wanajinusuru na hatari ya kushuka daraja, akieleza kuwa lengo lao ni kuepuka kabisa mechi za mchujo (play-off) ili kujipanga upya kwa msimu ujao.
“Singida Black Stars wameshikilia pakubwa hatma yetu. Tukivuka hapo salama huenda tukawa na furaha zaidi. Tunashukuru wachezaji wote tuna morali kubwa na kila mmoja anaipambania nembo ya Prisons,” alisema Sabiyanka.
“Pointi tulizonazo zinafikiwa na yeyote. Lazima tuwaheshimu wapinzani na tucheze kwa hesabu kubwa ili tumalize ligi salama, tuondoe presha kwa mashabiki na hata kwetu wachezaji.”
Aliwashukuru wadau na mashabiki wa Mbeya kwa sapoti yao na kuwaomba waendelee kuunga mkono timu hiyo katika kipindi hiki kigumu, akisisitiza kuwa kikosi kimejipanga kiufundi kuhakikisha kinabaki Ligi Kuu.