TANGU kiungo wa kati Jonas Mkude, alipoachana na Yanga msimu uliopita 2024-2025, amekuwa kimya kwa muda mrefu huku mwenyewe akisema anachokifanya hivi sasa ni kwa ajili ya kurejea kazini 2026-2027.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkude amesema, ingawa haonekani uwanjani kwa msimu huu 2025-2026, lakini anaendelea kujifua kwaajili ya kurejea msimu ujao, huku akificha jina la timu atakayoitumikia.

“Kwa msimu huu nimepumzika kidogo, ila sijapumzika kufanya majukumu yangu kama mchezaji ya kuzingatia miiko ya soka kama mazoezi ya kila siku ya kunikweka fiti, ili nikirejea kazini nisianze upya,” amesema Mkude na kuongeza:

“Kufanya mazoezi nje ya timu inahitaji moyo wa uvumilivu, lakini kwa kuwa natambua kazi yangu inahitaji kitu gani sioni ugumu wa hilo, badala yake naendelea na mapambano kama kawaida, kuna wakati nafanya ya kukimbia, beach (ufukweni) na gym.”

Mkude aliyetokea Simba B na kupandishwa timu ya wakubwa msimu wa 2011-2012 kisha akaichezea klabu hiyo hadi 2023, ndipo akajiunga na Yanga 2023 hadi 2025 alipomaliza mkataba, msimu huu 2025-2025 hana timu ya kuitumikia.

Kwa mujibu wa mtandao unaoorodhesha thamani za wachezaji duniani, Mkude alizaliwa Desemba 3, 1992 ambapo mwaka huu anatimiza miaka 34, jambo ambalo aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Moses Phiri raia wa Zambia, ameliambia Mwanaspoti kuwa bado nyota huyo wa zamani wa Simba ana umri wa kufanya vitu vingi dimbani.

Mchezaji huyo alimshauri Mkude aendelee kupambana na kuamini katika ndoto zake bila kujali mitazamo ya watu, kwani kuna wengine wanaweza kumkatisha tamaa.

Phiri aliyecheza Simba akiwa na Mkude kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, amesema: “Kuna wakati mchezaji anaweza akapitia changamoto ya kushuka kiwango na mashabiki wakamkatia tamaa, lakini anapaswa kujibu uwanjani kwa kucheza vizuri watamsapoti tu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *