Waziri wa michezo wa Italia, Andrea Abodi, amesema kuwa pendekezo la nchi yake kuchukua nafasi ya Iran kwenye Kombe la Soka la Dunia “si sahihi,” na akapinga wazo lolote kuwa timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Azzurri itapewa nafasi ya dharura katika mashindano ya ya soka ya FIFA mwaka huu.

Jumatano, iliripotiwa kuwa Paolo Zampolli, mjumbe maalum wa Rais wa Marekani Donald Trump, alipendekeza Italia ipewe nafasi ya haraka kwenye Kombe la Dunia licha kipigo kutoka Bosnia Herzegovina katika mechi za mchujo mwezi uliopita. Zampolli alipendekeza Italia, mabingwa mara nne wa dunia, wachukue nafasi ya Iran, akisema wana “hadhi na historia inayowastahili.” Lakini waziri wa michezo wa Irali amesisitiza kuwa mashindano ya Kombe la Dunia yanapaswa kuendelea kuwa ya wenye kustahili uwanjani.

Abodi ameiambia Sky News kuwa: “Pendekezo la Italia kurejeshwa kwenye Kombe la Dunia la 2026, kama ilivyodaiwa kupendekezwa na mjumbe wa Rais Trump, Paolo Zampolli, kwanza ni jambo lisilowezekana , na pili si jambo linalofaa,” akiongeza kuwa, “Kufuzu kunapaswa kuwa kwa mujibu wa matokeo uwanjani.”

Ushiriki wa Iran umekuwa ukitiliwa shaka kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Timu ya Taifa ya Iran inatarajiwa kucheza michezo miwili ya makundi mjini Los Angeles na mmoja Seattle. Ingawa Iran ilikuwa imetoa pendekezo la kuhamishia mechi zake nchini Mexico, mwenyeji mwenza , pendekezo hilo halikutekelezwa. Iran imetangaza nia ya kushiriki katika Kombe la Dunia na mwezi uliopita Rais wa FIFA, Gianni Infantino, alisema kuwa “Iran itakuwepo kwenye Kombe la Dunia.”

Rais wa Marekani Trump hapo awali alisema kuwa usalama wa timu ya taifa ya Iran huenda usiwe wa uhakika wakiwa Marekani. Tamko hilo lilikosolewa sana kwani nchi mwenyeji inapaswa kudhamini usalama wa timu zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *