
Ripoti ya kimataifa imeonya kwamba mzozo wa Mashariki ya Kati unaweza kuzidisha migogoro iliyopo, ikifichua kuwa watu milioni 266 katika nchi au maeneo 47 walikabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula mnamo 2025, karibu mara mbili ya idadi iliyorekodiwa mnamo 2016.
Ripoti ya “Hali ya Usalama wa Chakula Duniani 2026” – iliyotolewa na muungano wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na washirika wengine – imeonyesha kuwa theluthi mbili ya watu ambao walikabiliwa na migogoro ya chakula duniani mwaka jana wanaishi katika nchi 10 pekee.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi zilizokumbwa na njaa kali ni: Afghanistan, Bangladesh, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Myanmar, Nigeria, Pakistan, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen.
imedokeza kuwa migogoro inasalia kuwa kichochezi kikuu cha uhaba wa chakula, na kusababisha mateso kwa zaidi ya nusu ya watu wote wanaokabiliwa na njaa kali.
Imesema kuwa migogoro na mabadiliko makali ya hali ya hewa “huwenda yakaendeleza au kuzidisha hali hiyo katika nchi kadhaa,” na kufanya hali ya 2026 kuwa “yenye giza.”
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kumekuwapo ongezeko kubwa la njaa, huku zaidi ya watu milioni 39 katika nchi 32 wakikabiliwa na hali ya dharura ya uhaba wa chakula, na idadi ya watu wanaokabiliwa na janga la njaa ikiongezeka mara tisa tangu mwaka 2016.
Ripoti hiyo ya kimataifa imeonya juu ya kupungua kwa kasi ufadhili wa misaada ya kibinadamu, ikiongeza kuwa vita vya Mashariki ya Kati vinaweza kuzidisha migogoro iliyopo kwa kuongeza idadi ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo ambalo tayari linahifadhi mamilioni ya wakimbizi, pamoja na kupandisha bei ya mbolea.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema ripoti hiyo ni wito wa kuchukua hatua za kuimarisha dhamira ya kisiasa ili kuzidisha kasi ya uwekezaji katika misaada ya kuokoa maisha na kufanya kazi kwa ajili ya kukomesha migogoro.