HATIMAYE mshambuliaji wa Kitanzania, Clara Luvanga anayekipiga Al Nassr ya Wanawake, jana ameibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Saudia baada ya kuweka nyavuni mabao 24 kwenye mechi 14 alizocheza.
Huu ni msimu wa tatu kwa nyota huyo kuitumikia Ligi ya Saudia akijiunga na chama hilo mwaka 2023 akitokea Dux Lugrono ya Hispania alikodumu miezi mitatu.
Ndani ya misimu hiyo mitatu mbongo huyo alikuwa akikimbizana na kiatu cha ufungaji na nyota kutoka mataifa mbalimbali na hatimaye msimu huu amefanikiwa kuchukua kiatu.
Msimu wa kwanza Clara alifunga mabao 11 na asisti saba, uliofuata alifunga 21 na asisti saba na msimu huuu amevunja rekodi ya misimu mitatu akitikisa nyavu mara 24.
Katika mabao 24 aliyofunga aliweka hat-trick tatu, moja alifunga kwenye dabi dhidi ya mahasimu wao, Al Hilal na kuweka rekodi ya aina yake.
Ikumbukwe nyota huyo wa zamani wa Yanga Princess hakuwahi kuchukua kiatu cha ufungaji bora tangu aanze kucheza soka la kulipwa hivyo huu unakuwa msimu wake wa kwanza kubeba kwenye ligi akiwa nje.
Hii ni tuzo ya tatu kwa Clara kuchukua akiwa na Al Nassr, kwenye mashindano ya AFC mshambuliaji huyo aliibuka mfungaji bora kwa kuweka kambani mabao matatu sawa na mashindano ya SAFF Women Cup.
Pamoja na kiatu nyota huyo amebeba ubingwa wa tatu mfululizo akiwa na kikosi hicho ambacho msimu huu unakuwa wa nne kunyakua taji hilo mfululizo.