Dar es Salaam. Suala la wachuuzi wageni kufanya bishara zinazoweza kufanywa na wazawa limeendela kuwa mfupa mgumu, baada ya wafanyabiashara kuendelea kuilalamikia Serikali huku nayo ikiahidi kuwaondoa.

Malalamiko dhidi ya wachuuzi wageni na mengine yakiwemo masuala ya utiriri wa kodi, ymetolewa leo Aprili 25, 2026 na Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Severine Mushi kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka uliohudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga.

Miongoni mwa malalamiko ni uwepo wa wachuuzi wa kigeni kwenye soko la Kariakoo wanaofanya biashara zinazotakiwa kufanywa na wazawa, wingi wa kodi na barabara za Kariakoo kutopitika.

Hata hivyo, Waziri Kapinga amewahakikishia wafanyabiashara hao kuwa Serikali inajiandaa kuwaondoa kabisa wafanyabiashara wa kigeni wanaofanya biashara za uchuuzi.

Kapinga pia alieleza Serikali inajiaandaa kuanza utekelezaji wa mapendekezo ya kikosi kilichoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza na kuboresha masuala ya kodi kwa wafanyabiashara.

Kuhusu Kariakoo kufunga mitaa, amesema Serikali inafanya tathmini ili iboreshe barabara za mitaa ya Kariakoo ili kufungua soko.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga na Mbunge wa Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu (katikati) wakishiriki mkutano mkuu wa mwaka 2026 wa wafanyabiashara wa soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, Jumamosi Aprili 25, 2026.

Machi 18, 2025, Kamati ya kufuatilia na kuhakikisha Raia wa kigeni hawajihusishi na biashara zinazopaswa kufanywa na wazawa Kariakoo, Dar es Salaam, ilisema imewakuta wageni 152 wakifanya biashara katika maduka 75, huku 28 wakifanya kazi kinyume na vibali vyao.

“Kamati iliwakabidhi kwa Idara ya Uhamiaji na kati yao 24 waliondolewa nchini wakati kazi ikiendelea,” alisema Profesa Edda Lwoga, mwenyekiti wa kamati hiyo wakati akiwasilisha ripoti.

Alisema hata katika viwanda, wageni 106 walikuwa wanafanya kazi zisizohitaji utaalamu maalumu.

Hata hivyo, leo Waziri Kapinga amesema kero hizo zinafikia tamati, akiahidi kuchukua hatua kali dhidi ya hali hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika sokoni hapo, Kapinga amesema Serikali imeanza kushughulikia changamoto hizo, lakini mbinu zinazotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara wa kigeni zimekuwa zikibadilika kila Serikali inapochukua hatua.

“Tulishaanza kuchukua hatua, lakini wageni wamebadilisha mbinu. Tulikutana na wadau wametupa maoni, tupeni muda tunataka kuondoa kabisa hilo,” amesema Kapinga, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wafanyabiashara katika kutatua changamoto zao.

Kauli hiyo inakuja ikiwa imepita takriban mwaka mmoja tangu kuundwa kwa kamati ya kufuatilia na kuhakikisha Raia wa Kigeni hawajihusishi na biashara ndogondogo.

Kamati hiyo iliundwa na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo, kufuatia maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kuchunguza malalamiko ya wafanyabiashara Kariakoo.

Mbunge wa Ilala na Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu kwenye mkutano huo amewataka wafanyabiashara kupanua wigo wa biashara zao badala ya kujikita Kariakoo pekee.

 Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha mazingira ya amani na biashara yanakuwepo.

 “Amani ipo, na tutaendelea kuhakikisha inadumu, hivyo endeleeni kupanua biashara zenu msifikirie Kariakoo pekee,” amewashauri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *