Wakati Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Watu wa Asili, UNPFII, lililoanza Aprili 20 wiki hii kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani likiendelea hadi Mei Mosi mwaka huu, mpiga picha wa chombo hicho chenye wananchama 193 amevutiwa na unadhifu wa washiriki wengi kutokana na mavazi yenye rangi za kuvutia.

Mpiga picha huyo ameamua kupiga picha za studio zinazoangazia rangi tajiri na maelezo ya kipekee ya mavazi ya kitamaduni, akiamini kuwa mavazi haya yanadumisha maarifa ya kale kuhusu maisha, familia, na mazingira.

Miaka 25 ya UNPFII

Jukwaa hili, ambalo lilianzishwa mwaka 2000, mwaka huu linaadhimisha mwaka wa 25 tangu kuanzishwa kwake kama jukwaa la kipekee la kimataifa linalowakutanisha wadau kuhusu watu wa asili, huku likijikita katika mada za kuimarisha  afya, usawa na haki ya watu wa asili ya kujiamulia mambo yao wenyewe. 

Kupitia picha hizo ambazo ni miongoni mwa mkusanyiko wa Maktaba ya Picha ya Umoja wa Mataifa, ulimwengu unaalikwa kuacha upinzani dhidi ya yasiyojulikana na kukumbatia kufahamu utofauti wa tamaduni za binadamu.
Picha ya Umoja wa Mataifa/Manuel Elías Upande wa kushoto ni Aili Keskitalo (Biehttár-Heaikka Elle Máreha Áili) na upande wa kulia ni Runar Myrnes Balto (Biennáš Elle Eliasa Runar), wote kutoka kwa watu wa Sámi.

Mavazi yanayozungumza urithi wa utambulisho

Kutoka eneo la Sápmi linalounganisha Norway, Sweden, Finland, na Urusi, Aili Keskitalo na Runar Myrnes Balto ikitamkwa Biennáš Elle Elle Eliasa Runar, wamewakilisha watu wa jamii ya Sámi ambao idadi yao ni kati ya 50,000 hadi 80,000. 

Aili amevaa vazi la kitamaduni linaloitwa Gákti lenye mapambo ya fedha yanayoashiria utajiri na ulinzi, ambapo urembo wa kofia na mikono yake humtambulisha kuwa anatoka jamii ya Guovdageaidnu itamkwayo Kautokeino.

Runar naye amevaa Gákti inayowakilisha utamaduni wa markasámi, njia za mababu zake za kufuga kulungu (mnyama aina ya jamii ya swala), huku jina lake likiwa na neno “Elle” mara mbili ili kuwaenzi bibi na bibi mzaa bibi yake ambao wote waliitwa jina ‘Elle’.

Kutoka nchini Kenya, Silvia Museiya wa jamii ya Yiaku ikitamkwa Yaaku yenye watu 4,000 katika msitu wa Mukogodo, kaunti ya Laikipia ameonesha utambulisho wake wa asili.

Picha ya Umoja wa Mataifa/Manuel Elías Kwa upande wa kushoto ni Silvia Museiya, kutoka jamii ya Yaaku. kaunti ya Laikipia nchini Kenya na kulia ni Tina Ngata, wa jamii ya Ngāti Porou nchini New Zealand.

Tina kutoka New Zealand na chale na jino la nyangumi

Kwa upande mwingine, Tina Ngata wa watu wa jamii ya Ngati Porou kutoka Aotearoa nchini New Zealand, yenye wakazi 71,049, amevaa pambo la jino la nyangumi linaloitwa rei puta linaloashiria kuwa wao ni “watu wa nyangumi”.

Tina pia ana chale za moko kauae na uhi mwilini mwake zinazoonesha azma yake ya kulinda mito na jamii za asili.

Ufundi wa mikono katika mavazi

Kutoka Kaskazini mwa Vietnam, Samone Khouangsathiene na Matsalyn Baccam Brown wamewakilisha watu wa jamii ya Tai Dam ambao idadi yao inakaribia milioni moja. Wamevalia vilemba vya piew vilivyoshonwa kwa mkono ili kuwalinda na jua na upepo, pamoja na blauzi zenye vifungo vya fedha vilivyochongwa kwa maumbo ya maua, nyenje, na vipepeo.

Picha ya Umoja wa Mataifa/Manuel Elías Kwa upande wa kushoto ni Samone Khouangsathiene na kwa upande wa kulia ni Matsalyn Baccam Brown. Wote ni wa Tai Dam, kundi la wenyeji kutoka Meung Tai, mkoa katika eneo linalojulikana sasa kama sehemu ya Vietnam ya Kaskazini.

Mavazi yao yanachanganya shingo za duara za asili na zile za ‘V’ za kisasa, jambo linalodhihirisha jinsi urithi unavyoendelea kuishi.

Huko Ecuador, Mirian Masaquiza wa jamii ya Kichwa Salasaka yenye wakazi 5,400, amevalia vazi la sherehe linalojumuisha sketi nyeusi ya anaco, mkanda wa chumbi, blauzi ya pichu jirguita, na mtandio wa ucupachallina wenye mapambo ya rangi.

Manyoya ya tai na alama ya heshima Canada

Hatimaye, Chifu Mkuu, Wilton Littlechild kutoka jamii ya Cree nchini Canada yenye watu takribani 392,420, ameonesha kofia ya kitamaduni iliyotengenezwa kwa manyoya ya tai na nywele za farasi.

Picha ya Umoja wa Mataifa/Manuel Elías Kwa upande wa kushoto, Mirian Masaquiza, mwanamke asili wa Kichwa Salasaka kutoka eneo la Andean la Ecuado. Kulia, Chifu Mkuu Wilton Littlechild kutoka jamii ya Cree nchini Canada.

Kofia hii huvaliwa na viongozi wa kiume pekee, ambapo manyoya ya tai yanatazamwa kama alama ya juu kabisa ya heshima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *