
Vyanzo vya ngazi ya juu vya kimkakati katika kanda vimeeleza kuwa shehena ya zana za kijeshi iliyotoka katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel imesafirishwa hadi Somalia kwa jina la ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN).
Vyanzo hivyo vimeuambia mtandao wa al-Mayadeen wa Lebanon kuwa, shehena hiyo yenye uzito wa takriban tani moja (kilo 1,000), iliondoka Tel Aviv, kupitia Nairobi, na kutua Mogadishu mnamo Juni 21.
Taarifa hizo zimefichua kuwa shehena hiyo ilisajiliwa kama vifaa vinavyoelekea ofisi ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Imedokezwa kuwa shehena hiyo ilikuwa na “mfumo wa hali ya juu wa mawasiliano” uliokusudiwa kwa matumizi ya kijeshi na ujasusi.
Ripoti zinasema vifaa hivyo vya kijeshi vimeundwa na kampuni inayojulikana kama “Mer Security and Communications,” iliyopo katika mji wa Or Yehuda katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina, na ripoti zinasema shehena hiyo ilipokewa na ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Mogadishu.
Hivi karibuni kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul-Malik al-Houthi, alisema kuwa kundi hilo litachukua hatua madhubuti dhidi ya harakati zozote za kutaka kujitanua za Israel nchini Somalia.
Akizungumza mnamo Juni 25, Al-Houthi alisema kuwa Ansarullah “itachukua hatua za haraka wakati wowote ili kudhibiti shughuli za Israel katika ardhi ya Somalia na haitakaa kimya mbele ya sera za kutaka kujipanua za Israel katika Pembe ya Afrika.”
Amesema utawala wa Israel unatakka kujiimarisha nchini Somalia ili kudhibiti Ghuba ya Aden na Lango la Bab al-Mandab, ambayo ni njia kuu ya kimkakati ya usafirishaji wa baharini duniani.
Kiongozi huyo wa Ansarullah nchini Yemen alitoa wito kwa nchi zinazopakana na Bahari ya Shamu kuchukua msimamo wa pamoja na imara dhidi ya uingiliaji wa Israel katika kanda hiyo, hatua inayotazamiwa kuongeza mvutano wa kijeshi na kiiusalama katika eneo hilo la kimkakati.