KATIKA kikosi cha Mashujaa, licha ya kuwa na washambuliaji wenye uzoefu na Ligi Kuu Bara, lakini linapokuja suala la kucheka na nyavu, kumekuwa na changamoto hali inayofanya viungo nao kuchukua jukumu hilo.

Si Danny Lyanga, Mudathir Said, Crispin Ngushi, wala Ismail Mgunda waliofunga mabao, badala yake, kati ya mabao 10 yaliyofungwa na timu hiyo, kuna viungo waliohusika na manne ambao ni Abdul Bakari, Hassan Haji, Idrisa Stambuli na Mgandila Shaban, huku moja likitoka kwa beki Baraka Mtuwi.

Hata washambuliaji waliofunga mabao ndani ya kikosi hicho, namba zao haziridhishi kwani Jafari Kibaya na Mundhir Vuai kila mmoja amefunga mawili, wakati Nyenyezi Shabani akiwa na moja.

Kwa upande wa asisti, hapa unakutana na Ngushi na Mudathir ambao ni washambuliaji, wakati viungo ni Selemani Bwenzi, David Ulomi na Salum Kihimbwa ambao kila mmoja ametengeneza moja.

VIU 01

Mashujaa kwenye mechi tisa ilizopata sare, sita haijafunga bao lolote na kuonyesha eneo la washambuliaji bado lina changamoto kubwa.

Wanajeshi hao wamepoteza mechi sita hadi sasa na tano haijafunga bao lolote, huku moja pekee ikifunga la kufutia machozi ilipopoteza 2-1 ugenini dhidi ya Pamba Jiji lililofungwa na Mtui.

Kocha wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ akizungumzia hilo, amesema wamekuwa wakilifanyia kazi eneo la ushambuliaji na anaamini wakati wowote wataimarika na kuanza kufunga kwa kasi.

VIU 02

“Timu wakati naikuta ilikuwa inacheza kwa presha sana, hivyo changamoto kama hizo lazima zijitokeze, lakini tumekuwa tunayafanyia kazi hayo kila wakati, unaona timu inatengeneza nafasi, shida ilikuwa utulivu, naamini kwa kazi ambayo tumeifanya watabadilikka hivi karibuni, nawaamini sana wachezaji wangu,” amesema Julio.

Mashujaa inashika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 19, imeshinda nne, sare tisa na kupoteza sita, ikikusanya pointi 21, imefunga mabao 10 na kuruhusu 17.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *