FAO nchini Kenya inasema mradi huo wa miaka mitano uitwao FARM, unalenga kuimarisha uwekezaji katika mbinu mbadala na usimamizi endelevu wa kemikali hatari na plastiki kwenye sekta ya kilimo barani Afrika na Amerika ya Kusini.

Ukifadhiliwa na Fuko la Mazingira Duniani, GEF, mradi unafanya kazi na vikundi vya wataalamu wa kitaifa kutoka taasisi mbalimbali, kuangazia vipaumbele na changamoto za ndani ili kutengeneza mitaala ya mafunzo inayolinda mazingira.

Ripoti ya mradi imebainisha kuwa matumizi ya viuatilifu yamekuwa na madhara makubwa kwa viumbe wanaosaidia uchavushaji wa mimea. Aidha, mabaki ya sumu hizi yanaweza kukaa kwenye udongo kwa zaidi ya miaka 30, jambo ambalo ni hatari sio tu kwa mazao ya chakula bali pia kwa afya za wakulima. 

Madhara ya matumizi kupita kiasi

Matumizi yaliyopitiliza yamehusishwa na magonjwa ya saratani na matatizo ya mfumo wa mishipa ya fahamu, huku yakipunguza uwezo wa nchi kuuza mazao yao kwenye masoko ya kimataifa kutokana na viwango vya sumu kuzidi mipaka ya usalama wa chakula. 

Afisa wa FAO, Oxana Perminova anasema, “plastiki na kemikali za kilimo ni jambo linalotia wasiwasi duniani kote. Suala hilo limekuwa katika ajenda za nchi nyingi. Kwa upande wa Kenya, tunaamini kuwa ushirikiano huu ambao umeanzishwa hapa na ambao kwa kweli unafanya kazi ya na unawaleta wadau wote pamoja utakuwa na manufaa makubwa kwa kanda hii. Hivyo nchi nyingine jirani zinaweza kuangalia mifano na bidhaa zitakazozalishwa ndani ya ushirikiano huu na kuzitumia mahususi kwa ajili ya kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na kemikali na plastiki za kilimo na kuwalinda wakulima, hasa katika maeneo haya.” 

Fahamu kuhusu madhara ya plastiki za vifungashio

Kuhusu plastiki za vifungashio vya pembejeo za kilimo, takwimu zinaonesha kuwa takriban tani 330,000 za plastiki hutumika kila mwaka kama vifungashio vya viuatilifu duniani kote.

Inakadiriwa kuwa asilimia 35 ya plastiki hizi hazidhibitiwi ipasavyo, ambapo asilimia 10 huishia baharini na nyingine nyingi kubaki kwenye udongo.

Grace Muchemi, ni Meneja Mkuu wa bodi ya kudhibiti bidhaa za viuatilifu, PCPB, nchini Kenya, anaeleza hatua zinazochukuliwa kuwa ni “tunapotazamia njia mbadala salama zaidi, tumekuwa tukipitia upya viuatilifu ili kuhakikisha viuatilifu vyenye hatari ndogo vinatumika ndani ya nchi. Pia, utoaji wa uelewa umefanyika ndani ya kaunti, na tunafanya kazi pamoja na mashirika mengine ya serikali na pia wadau wa maendeleo kutoa uelewa juu ya matumizi salama ya viuatilifu ili kuhakikisha chakula salama na pia kuwezesha biashara na nchi nyingine.”

Katika hatua muhimu ya kuleta usawa, mradi huu umehakikisha uwiano sawa wa washiriki wanaume na wanawake katika mafunzo yote yatakayotolewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *