Katika mahojiano na Idhaa ya Kiingereza ya Umoja wa Mataifa kabla ya kikao muhimu cha Baraza la Usalama leo Jumatatu kuhusu usalama wa baharini, Dominguez amesema kuwa kuzuiwa kwa meli katika Mlango wa Bahari wa Hormuz kufuatia mvutano kati ya Marekani na Iran kumewaacha hadi mabaharia 20,000 wakiwa wamekwama ndani ya takriban meli 2,000 katika Ghuba ya Uajemi, bila uwezo wa kupita salama katika njia hiyo nyembamba ya maji.

Amesisitiza kuwa hali hiyo inaonesha wazi jinsi sekta ya usafiri wa baharini ilivyo hatarini katika maeneo yenye migogoro. “Meli na wafanyakazi wake wanajikuta katikati ya migogoro ambayo si yao, na mara nyingi hutumiwa kama chombo cha shinikizo katika mvutano wa kisiasa,” amesema.

Usalama baharini ni nini?

Akifafanua dhana ya usalama wa baharini, Dominguez amesema unahusisha ulinzi wa meli, bandari, mabaharia na miundombinu ya baharini dhidi ya vitisho kama uharamia, ugaidi na mashambulizi ya mtandao. 

©IMO/Marco Theo G. Caliwag Baharia akiwa kazini ndani ya meli baharini.

Pia unajumuisha mapambano dhidi ya shughuli haramu kama usafirishaji wa silaha na dawa za kulevya, biashara haramu ya wanyamapori, usafirishaji haramu wa binadamu na utupaji wa taka hatari baharini.

“Usalama wa baharini ni muhimu kwa sababu unalinda biashara ya kimataifa, unahakikisha usalama wa mabaharia na kudumisha minyororo ya usambazaji wa bidhaa. Bila usalama wa baharini, maendeleo ya sekta hii yanasimama, na bila maendeleo hayo, maendeleo endelevu hayawezekani,” amesisitiza.

Hatari zinazoibuka na mabadiliko ya vitisho

Dominguez ameeleza kuwa vitisho dhidi ya usalama wa baharini vimebadilika kwa miaka, kuanzia utekaji wa meli ya kitalii ya Italia mwaka 1985 hadi mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001, ambayo yalionesha uwezekano wa meli kutumika kama zana ya ugaidi.

Katika miaka ya hivi karibuni, matukio ya uharamia, hasa katika Pembe ya Afrika na Ghuba ya Guinea, yamekuwa changamoto kubwa. Hata hivyo, vitisho vipya vinaibuka, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mtandao dhidi ya mifumo ya urambazaji na mizigo, uharibifu wa miundombinu ya chini ya bahari kama nyaya na mabomba, pamoja na mashambulizi yanayotumia ndege zisizo na rubani dhidi ya meli.

Aidha, ameonya kuwa wahalifu wanazidi kuwa na mbinu za kisasa katika kuvuruga minyororo ya usambazaji wa bidhaa kimataifa.

Mabaharia sio walengwa wa vita

Akizungumzia changamoto ya kulinda mabaharia, Dominguez amesisitiza kuwa mabaharia wa kiraia si wapiganaji na hawapaswi kuwa walengwa wa mashambulizi. “Meli nyingi za kibiashara hazina uwezo wa kujilinda dhidi ya mashambulizi ya kisasa kama makombora au ndege zisizo na rubani,” amesisitiza.

Amependekeza kuwa kubadilishana taarifa sahihi, tathmini za hatari kabla ya safari na juhudi za kidiplomasia za kupunguza mvutano ni hatua muhimu za kulinda sekta hiyo na kwamba, “kusindikizwa jeshi la wanamaji si suluhisho la kudumu.”

© IMO/Vincent Dwight Rafil Usafirishaji wa bidhaa duniani unaweza kuvurugika iwapo meli hazitakuwa na uhuru wa kurambaza baharini

Njia muhimu za bahari hatarini

Dominguez ametaja maeneo muhimu ya usafiri wa baharini duniani ambayo yanaweza kuathiriwa vibaya kwa urahisi wakati wa migogoro, ikiwa ni pamoja na:

  • Mfereji wa Suez
  • Mlango Bahari wa Bab el-Mandeb
  • Mlango wa Bahari wa Hormuz 
  • Mlango wa  Bahari wa Malacca
  • Singapore
  • Mfereji wa Panama

“Usumbufu katika maeneo haya unaweza kuwa na athari mbaya kubwa kwa biashara ya kimataifa na usalama wa chakula duniani,” ameonya.

Jukumu la Umoja wa Mataifa

Kuhusu mchango wa Umoja wa Mataifa, Dominguez amesema IMO inashirikiana na washirika wa kimataifa kusaidia nchi kujenga uwezo wa kukabiliana na vitisho vya usalama wa baharini. 

“Hii inajumuisha kuboresha sheria, kuimarisha ushirikiano wa kikanda, na kukuza ubadilishanaji wa taarifa.”

Amesisitiza pia umuhimu wa sheria za kimataifa katika kuhakikisha uhuru wa urambazaji wa meli, pamoja na juhudi za kidiplomasia na kibinadamu za kulinda mabaharia na kudumisha utulivu katika bahari za dunia.

“Hatuwezi kuruhusu mabaharia wa kiraia kuwa waathiriwa  wa migogoro ya kisiasa. Usalama wao ni jukumu la pamoja la jumuiya ya kimataifa,” ametamatisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *