Rombo. Serikali, kupitia Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), imeanza kuhuisha maktaba za vijiji zaidi ya 2,900 zilizokuwa hazitoi huduma zilizokusudiwa kwa jamii.
Lengo ni kuendana na mfumo mpya unaozingatia mahitaji ya kisasa katika jamii.
Hayo yamesemwa leo, Aprili 27, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB), Dk Mboni Ruzegea, wakati wa uzinduzi wa maktaba ya jamii katika Shule ya Sekondari Bustani, iliyopo Kata ya Mrao-Keryo, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, iliyogharimu zaidi ya Sh202 milioni.
Dk Mboni amesema maktaba hizo, ambazo zilianzishwa miaka ya 1980, zilikuwa ni sehemu ya dhamira pana ya Taifa ya kujenga jamii yenye kujua kusoma, kujifunza na kutumia maarifa wanayopata katika kujiletea maendeleo yao binafsi.
“Maktaba nyingi katika nchi yetu zimekuwa hazitoi huduma ipasavyo kutokana na uchakavu na ukosefu wa miundombinu. Aidha, katika maeneo mengine kuna uhaba wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia. Vilevile, kuna upungufu wa wataalamu wanaosimamia maktaba hizi, hasa katika maktaba za shule na vituo vya elimu. Kutokana na hali hiyo, maktaba nyingi zinatumika kama vyumba vya kuhifadhia vitabu katika sehemu nyingi,” amesema Dk Mboni.
Aidha, amesema Serikali, kwa kutambua hilo, imeanza kuhuisha dhamira yake kwa kuweka mfumo mpya unaozingatia mahitaji ya kisasa ya kijamii ili lengo lililokusudiwa liweze kutimia.
“Maktaba za kijamii zinaimarishwa sasa ili ziendane na ajenda pana ya elimu, ili kuweza kukidhi matumizi ya Tehama, upatikanaji wa ujuzi na ujifunzaji. Mwelekeo wa wizara sasa ni kufanya maktaba hizi kuwa sehemu muhimu ya miundombinu ya elimu hapa nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Hussein Omar, akikagua vitabu katika maktaba ya Shule ya Sekondari Bustani, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, mara baada ya kuzindua maktaba hiyo.
“Katika kujengea watu utamaduni wa kupenda kusoma, bodi ina mikakati ya kugeuza maktaba hizi za jamii kuwa vituo hai vya maarifa vinavyowezesha wananchi kutunza historia, mila na desturi zao,” amesema Dk Mboni.
Pamoja na mambo mengine, amesema bodi hiyo imeipatia maktaba hiyo jumla ya vitabu 690 vyenye thamani ya zaidi ya Sh11 milioni, lengo ikiwa ni kukuza ujuzi na maarifa mbalimbali ya wasomaji.
Naye, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Hussein Omar, ameipongeza bodi hiyo kwa hatua hiyo kubwa na kuitaka jamii kutumia maktaba hiyo kwa ajili ya kupata maarifa mbalimbali.
“Tunaipongeza Bodi ya Huduma za Maktaba nchini kwa kuwa na maktaba za jamii katika maeneo mbalimbali nchini. Nitoe rai kwa jamii tutumie maktaba hii, lakini wazazi mtusaidie vijana wetu waweze kujifunza, kwani haya ni mapinduzi makubwa yanayofanyika katika sekta ya elimu hapa nchini,” amesema Dk Omar.
Akizungumza, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Gilbert Tarimo, amesema ujenzi wa maktaba hiyo ya kisasa utasaidia kuweka mazingira mazuri kwa wanajamii kujifunza na kupata maarifa mapya yatakayowasaidia katika mambo mbalimbali.
“Maktaba hii ina mazingira mazuri kwa ajili ya wanajamii kujisomea na kupata maarifa mbalimbali. Pia, natambua kuwa maktaba hii itakuwa ya kidijitali, itatumia vitabu vya mtandaoni, na itakuwa rahisi kupatikana vitabu mbalimbali vitakavyosaidia jamii yetu,” amesema Tarimo.
Mwanaidi Bakari na Irene Damas, ambao ni wanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, wamesema uwepo wa maktaba hiyo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunza na kuwaongezea maarifa zaidi katika masomo yao.