Hai. Mwanaume ambaye hajafahamika majina wala umri amefariki dunia kwa kuzama katika Mto Sanya wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, akidaiwa kuteleza alipokuwa akivuka kivuko cha magogo kinachotumiwa na wananchi kama njia ya muda.
Tukio hilo limetokea leo Aprili 27, 2026, katika mtaa wa Masinonda, kata ya Masama Kusini, likiacha simanzi kwa wakazi wa vijiji vya Mungushi (Hai) na Munge (Siha) vinavyounganishwa na mto huo.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremia Mkomagi, amesema walipokea taarifa ya tukio hilo saa 2:23 asubuhi na kufika eneo la tukio saa 5:38, na walikuta mwili wa mwanaume huyo ukielea juu ya maji.
Amesema askari hao walifanikiwa kuuopoa mwili huo saa 7:15 mchana na kuukabidhi kwa Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo cha tukio.
“Mwili ulikutwa ukielea juu ya maji katika Mto Sanya na haukutambulika mara moja. Tumeukabidhi kwa Polisi kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi zaidi,” amesema Mkomagi.
Akizungumza katika eneo la tukio, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mungushi, Lameck Simbo amesema eneo hilo halina kivuko rasmi na wananchi hulazimika kutumia gogo lililokwama kuvuka mto huo.
“Pale hakuna kivuko salama, wananchi wanatumia gogo kama daraja la muda. Inawezekana marehemu aliteleza wakati akivuka,” amesema Simbo.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakiwa katika Mto Sanya, wilayani Hai.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Munge, wilayani Siha, Izack Mollel amesema eneo hilo limekuwa hatarishi kutokana na kasi ya maji na mmomonyoko wa ardhi, hali inayohatarisha maisha ya watumiaji wa kivuko hicho.
“Hii ni njia muhimu kwa shughuli za kila siku za wananchi, lakini imegeuka kuwa hatari. Tunaiomba Serikali itujengee daraja la kudumu ili kuokoa maisha,” amesema Mollel.
Wananchi wanaotumia kivuko hicho wamesema wamekuwa wakivuka kwa hofu, wakitaka hatua za haraka zichukuliwe.
Mkazi wa Mungushi, Paulo Mrema, amesema hulazimika kuvuka kila siku kwenda mashambani licha ya hatari iliyopo.
“Hapa ni hatari sana, hasa wakati wa mvua. Tunavuka kwa uoga mkubwa, lakini hatuna namna kwa sababu hii ndiyo njia yetu. Tunaomba Serikali itusaidie kupata daraja,” amesema.
Naye mkazi wa Munge, Neema Mushi, amesema wanawake na watoto wako kwenye hatari zaidi wanapotumia kivuko hicho.
“Unavuka ukiwa na hofu muda wote. Maji yakiongezeka kidogo tu, hali inakuwa mbaya zaidi. Tunaomba kivuko salama kijengwe ili kuepusha vifo kama hivi,” amesema.
Wakati huo huo, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha uwepo wa mvua kubwa kwa siku mbili mfululizo kuanzia leo katika baadhi ya mikoa ikiwemo Kilimanjaro, hali inayoweza kuongeza hatari ya mafuriko na ajali katika maeneo yenye mito.
TMA imewataka wananchi kuchukua tahadhari ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.