
Same. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Boniphace Olenjoro (47), dereva wa gari dogo aina ya Toyota Land Cruiser, kwa kusababisha ajali iliyosababisha vifo vya watu watatu na majeruhi wawili katika barabara kuu ya Tanga/Moshi–Arusha, wilayani Same.
Ajali hiyo ilitokea Jumapili, Aprili 26, 2026, saa sita usiku, baada ya dereva wa gari hilo kudaiwa kuhama upande wake wa barabara na kugongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Tahmeed lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Nairobi, Kenya.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Simon Maigwa, amethibitisha kukamatwa kwa dereva huyo leo, Aprili 27, 2026, amesema atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Amesema ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser mali ya shirika la OIKOS East Africa, lililokuwa likitoka Same mjini kuelekea Tanga, ambalo lilihama upande wake na kugongana na basi la kampuni ya Tahmeed lililokuwa likitokea Dar es Salaam kwenda Nairobi.
Kamanda Maigwa amewataja waliofariki dunia kuwa ni Fridorin Leonard Ziku (30) mkazi wa Njombe, Ekasia Walter Minja (28) mkazi wa Arusha na Tumaini Laizer (28) mkazi wa Loliondo, mkoani Kilimanjaro.
Aidha, majeruhi katika ajali hiyo ni Groria Samwel Laizer (25) mkazi wa Arusha na Erick Ngonga Otieno (38) mkazi wa Nairobi, Kenya.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia dereva wa gari aina ya Toyota Land Cruiser kwa kusababisha ajali iliyosababisha vifo vya watu watatu na majeruhi wawili na uharibifu wa mali,” amesema Kamanda Maigwa na kuongeza kuwa majeruhi wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mji Same.