
Mvomero. Hospitali ya Wilaya ya Mvomero imeanza kutoa huduma za kibingwa ikiwamo upasuaji wa jumla baada ya Serikali ikiwekeza Sh5.2 bilioni kwenye ujenzi wa hospitali hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2015 na kuanza kutoa huduma mwaka 2017.
Akitoa taarifa ya utoaji ya huduma za afya jana Jumapili Aprili 26, 2026 kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah aliyefanya ziara hospitalini hapo, Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya kina mama, Dk Revocatus Chuma amesema kutokana na kuwepo kwa huduma za kibingwa idadi ya wagonjwa wanaofika hospitalini hapo imeongezeka kutoka 100 hadi 120 kwa siku.
Amesema mbali ya kutoa huduma za kibingwa lakini pia Serikali imepeleka vifaa tiba vya kisasa hospitali hapo zikiwamo mashine za vipimo vya X-ray na Utra Sound.
Amesema mpaka sasa hospitali hiyo ina uwezo wa kutoa vipimo 98 vya magonjwa mbalimbali kikiwamo kipimo cha saratani ya matiti.
“Tayari tuna jengo la kufanyia vipimo vya mionzi, jengo hili lina vifaa vyote, tumepokea mashine maalumu kwa ajili ya kupima saratani ya matiti na mpaka sasa wagonjwa 3,625 wameshapata vipimo,” amesema Dk Chuma.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Philipina Philipo amesema wananchi wa wilaya ya jirani ikiwamo Gairo na Kilosa ambao wamekuwa wakifika hospitalini hapo kupata matibabu.
Dk Philipo amesema Serikali imeendelea kupanua hospitali hiyo kwa kujenga majengo ya kisasa ya kutolea huduma.
Amesema hospitali hiyo inapaswa kuwa na majengo 32, hivyo mpaka sasa tayari majengo 17 bado yanaendelea kujengwa.
Kuhusu idadi ya watumishi, Dk Philipo amesema hospitali hiyo ina jumla ya watumishi 91 na kati ya hao madaktari bingwa ni watatu akiwamo wa kina mama na upasuaji wa jumla.
Akieleza changamoto zilizopo hospitalini hapo Dk Philipo amesema ni pamoja na kukosekana kwa gari kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa hospitali hasa katika utoaji wa chanjo ya mkoba na kukosekana kwa maji ya bomba.
Kufuatia changamoto ya maji Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adamu Malima amewataka Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) kufika haraka hospitalini hapo na kufanya utafiti kujua ni eneo gani la hospitali hiyo linaweza kuchimbwa kisima kirefu na kupata maji kwa ajili ya matumizi ya hospitali hiyo.
“Wakati tunasubiri hawa kina Moruwasa waweze kuleta maji hapa, nataka Ruwasa mje mfanye utafiti wa kujua wapi kuna mwamba utakaotoa maji,” amesema Malima.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah mbali ya kutembelea hospitali hiyo ya Wilaya Mvomero lakini pia alikagua mradi wa ujenzi wa stendi ya daladala inayojengwa jirani na Stesheni ya SGR pamoja na mradi wa upanuzi wa majengo ya Chuo cha Ualimu Dakawa kilichopo Wilaya ya Kilosa.