
Suala hilo la mchango wa manusura katika kuepusha mauaji kama hayo hayajirudii tena, nililimulika wakati wa mazungumzo yangu ya hivi karibuni na Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi
Martin Ngoga ambaye bila kumung’unya maneno alinieleza kuwa, “ wanamchango mkubwa sana kwa sababu kwanza wanapambana na hali ambayo katika hali ya kawaida ya ubinadamu ni ngumu. Chukulia mfano wetu sisi Rwanda walionusurika mauaji na waliotekeleza wanaishi pamoja kwa sababu Rwanda hakuna mgawanyiko wa kikabila wa kwamba kuna baadhi wanaishi mkoa fulani. Wanaishi pamoja katika vijiji hivyo, hivyo wanaenda shule hizo hizo wanaenda hospitali pamoja na wanaishi pamoja. Kwa mtu ambaye amepoteza familia yake nzima na anawajua wauaji walioua familia yake na anaendelea kuishi nao kijijini, ni hali ambayo kwa kweli katika akili ya kawaida unaweza usielewe lakini imetokea Rwanda.”
Mwaka huu wa 2026 ni miaka 32 tangu kutokea kwa mauaji hayo ya kimbari. Hivyo Balozi Ngoga ambaye aliwahi kuwa Mwakilishi wa Rwanda kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu uliotokea Rwanda (ICTR) akafafanua kwamba, “Baadhi ambao walikuwa ni wadogo wakati huo ambao sasa ni watu wazima, wanaandika hata vitabu kueleza nini kilitokea. Lakini wamekubali kuingia katika mchakato wa maridhiano, kujenga upya taifa la Rwanda.”
Akaongeza kuwa, “na kama ambavyo aliwahi kusema kiongozi wetu Rais Paul Kagame wakati fulani kwamba wao walionusurika ndio wanacho cha kutoa. Wao ndio wanaombwa watoe zaidi katika kuchangia juhudi za kulijenga upya taifa kwa sababu muuaji unaenda kumuomba nini. Tunashukuru kwamba wamekubaliana na hiyo, hali ambayo katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu ni ngumu sana. Lakini kwa miaka yote hii tunakwenda.”