Dodoma. Wakati dunia ikiendelea kushuhudia mapinduzi ya sayansi na teknolojia, Tanzania imeanza kunufaika na matumizi ya teknolojia ya uchunguzi wa vinasaba (DNA), huku Serikali ikieleza kuwa hatua hiyo inaleta matumaini mapya katika sekta ya afya, haki jinai na uhifadhi wa rasilimali za Taifa.

Katika kile kinachoonekana kuwa zama mpya za matumizi ya sayansi katika maisha ya kila siku, Serikali imesema teknolojia ya DNA si tu imeongeza ubora wa huduma za afya, bali pia imekuwa silaha muhimu katika vita dhidi ya uhalifu, ujangili na majanga.

Akifungua maadhimisho ya Siku ya Vinasaba Tanzania 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Teknolojia ya DNA imeleta mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwa kusaidia utambuzi sahihi wa magonjwa, upandikizaji wa viungo, tiba jeni na hata maendeleo ya chanjo za kisasa,” amesema.

Mbali na sekta ya afya, amesema uchunguzi wa vinasaba sasa unatumika kama ushahidi muhimu katika kesi za jinai, ukisaidia kubaini wahusika wa uhalifu au kuwaondolea hatia watu wasiohusika.

Katika mapambano dhidi ya ujangili, teknolojia hiyo pia imekuwa msaada mkubwa kwa kubaini aina ya wanyama waliouawa, jinsia zao pamoja na kuwahusisha watuhumiwa na makosa husika.

Serikali imewekeza zaidi ya Sh16 bilioni katika kuimarisha miundombinu ya maabara za kisasa pamoja na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi wa vinasaba, hatua inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha matumizi ya teknolojia hiyo Afrika Mashariki.

Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko, amesema kwa zaidi ya miaka 20 sasa, teknolojia ya DNA imekuwa nyenzo muhimu nchini, huku takwimu zikionesha kuwa sampuli 8,956 zilichunguzwa kati ya Januari 2025 na Machi 2026 pekee.

Mkemia Mkuu wa Serikali Dk Fidelice Mafumiko.

Kwa mujibu wa Dk Mafumiko, uchunguzi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za kijamii, kesi za kifamilia, migogoro ya kisheria na masuala ya kiuchumi.

Wataalamu wanaamini kuwa maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Kufungua Fursa kwa Jamii kupitia Uchunguzi wa Vinasaba” yanaashiria mwanzo wa Tanzania mpya inayotumia sayansi kama msingi wa maendeleo, huku jamii ikitakiwa kuelewa zaidi umuhimu wa teknolojia hiyo katika maisha ya sasa na baadaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *