Longido. Serikali imeahidi kutoa zaidi ya Sh700 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la kisasa katika Shule ya Sekondari Longido iliyopo Wilaya ya Longido mkoani Arusha, ikiwa ni hatua ya kumaliza changamoto ya muda mrefu ya msongamano wa wanafunzi zaidi ya 3,000 wanaotumia bwalo dogo lisilokidhi mahitaji yao.
Ahadi hiyo imetolewa Aprili 26, 2026 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia Elimu, Dk Festo Dugange wakati akizungumza kwenye mahafali ya 21 ya kidato cha sita yaliyofanyika shuleni hapo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wanafunzi wa kidato cha sita kuwasilisha risala maalumu iliyoeleza changamoto kubwa ya ukosefu wa bwalo lenye uwezo wa kuwahudumia wanafunzi wote, hali inayosababisha usumbufu mkubwa wakati wa chakula pamoja na shughuli nyingine za kijamii na kitaaluma.
Akijibu ombi hilo, Dk Dugange amesema Serikali imepokea kwa uzito changamoto hiyo na imejipanga kuhakikisha mazingira ya shule hiyo yanaboreshwa kwa kiwango cha kisasa.
“Serikali imewasikia, tumejipanga kutoa zaidi ya Sh700 milioni kwa ajili ya ujenzi wa bwalo jipya litakalokidhi mahitaji ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Longido,” amesema Dk Dugange.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Longido
Amesema uwekezaji huo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya elimu kwa kuboresha miundombinu ya shule nchini.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, Serikali inaendelea kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira rafiki yatakayowawezesha wanafunzi kujifunza katika hali bora zaidi, sambamba na kuongeza ubora wa elimu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Salum Kalli, ameishukuru Serikali kwa hatua hiyo, akieleza bwalo hilo litakuwa suluhisho la kudumu kwa changamoto iliyokuwa ikiikabili shule hiyo kwa miaka mingi.
Pamoja na pongezi hizo, Kalli amewataka wanafunzi wanaotarajia kufanya mitihani ya taifa ya kidato cha sita kuendelea kusoma kwa bidii, kuzingatia nidhamu na kutumia vyema muda uliobaki kabla ya kuanza kwa mitihani Mei 4, 2026.
Mkuu wa Shule hiyo, Justine Swai amesema walimu wamejipanga kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri katika mitihani yao, akiongeza kuwa mazingira bora ya kujifunzia yataongeza ari na mafanikio zaidi kwa wanafunzi.
Uamuzi huo wa Serikali umeibua matumaini mapya kwa wanafunzi, walimu na wazazi wa Sekondari ya Longido huku ukitajwa kuwa hatua muhimu katika kuinua kiwango cha elimu wilayani humo.