Dodoma. Serikali imeagiza waajiri kulipa michango ya watumishi wao katika mifuko ya hifadhi kwa wakati, na kusisitiza kuwa wasiolipa makato hayo wafuatiliwe na sheria ichukue mkondo wake.

Kwa upande wa watumishi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), wameagizwa kuendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ili wajiunge kwa ajili ya maisha yao ya baadaye, akisisitiza mpango wa Hifadhi Skimu, ambako hadi Machi 30, 2026 walikuwa na wanachama 560,000.

Maagizo hayo yametolewa leo, Jumatatu Aprili 27, 2026, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, wakati akifungua Mkutano wa 56 wa Baraza la Wafanyakazi wa NSSF.

Waziri amesema Serikali haitamvumilia kuona watumishi wakitembelea kwenda ofisi za NSSF kuangalia michango yao wakati si jukumu lao, kwani kazi hiyo inapaswa kufanywa na NSSF.

Waziri Sangu amesema ipo tabia kwa baadhi ya waajiri kutopeleka michango ya watumishi kwa wakati kwenye mishahara yao, huku wakiwa wamekata, lakini kwa makusudi au kwa kuamua, wanavunja sheria, jambo alilosema halivumiliki.

Kiongozi huyo amebainisha kuwa baadhi ya waajiri ni kama wanajizima data kwa kuacha kutuma michango ya watumishi wao.

Waziri ameupongeza uongozi wa NSSF kwa makusanyo ya michango kutoka kwa waajiri, ambapo kiasi cha Sh341.67 bilioni kilikuwa kikidaiwa, lakini kwa muda mfupi mfuko umekusanya Sh253 bilioni, sawa na asilimia 74 ya madai, akiwaelekeza kiasi kilichobakia kikusanywe haraka.

“Waajiri ambao hawataki kulipa michango ya wafanyakazi wao lazima washughulikiwe kwa mujibu wa sheria, lakini endeleeni kutoa elimu ili watu wengi wajiunge na mfuko huu kwa manufaa yao na Taifa. Pia endeleeni kuwekeza kwenye miradi ya tija,” amesema Waziri Sangu.

Katika hatua nyingine, Waziri amesisitiza weledi na nidhamu katika utumishi kuwa muhimu, na watumishi waache kufanya kazi kwa mazoea, kwani Serikali inaendelea kuwajali, huku akitaja mkakati wa uhakiki ili kulipa deni la Sh1.4 trilioni ambalo Serikali inadaiwa na mfuko.

Kuhusu ongezeko la michango, Waziri ametaja sababu kuwa inatokana na ongezeko la mishahara, hasa katika sekta binafsi, jambo lililofanya taasisi hiyo iongeze kiwango cha makusanyo kwa kipindi kifupi.

Kuhusu uwekezaji, amesifu ujenzi wa hoteli katika miji ya Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam, pamoja na uwekezaji wa kiwanda cha sukari cha Mkulazi ambacho wakati wowote kitaanza uzalishaji.

Mkurugenzi wa NSSF, Masha Mshomba, ametaja mafanikio katika thamani ya mfuko, ambapo kipindi cha Juni 2020 walikuwa na Sh4.33 trilioni, lakini hadi Machi 30, 2026 wameongeza kiwango cha makusanyo na kufikia Sh11.5 trilioni.

Mshomba ametaja mafanikio hayo yamewezesha kulipa mafao ya watumishi kwa haraka, licha ya sheria kutaka iwe ndani ya siku 60, lakini mara nyingi wanalipa chini ya muda huo kutokana na uwezo wa kuwa na kumbukumbu sahihi.

Amesema ndani ya taasisi hiyo itaendelea kufanya kazi kwa kufuata misingi na maelekezo ya kisheria ili kujenga imani kwa wananchi na wanachama wake.

“Ndiyo maana tumeamua kuwekeza zaidi katika Tehama. Tunafanya hivyo ili kuhakikisha tunakuwa na ulinzi wa taarifa zetu, lakini pia kuwa na uwazi pindi mtumishi anapotakiwa kulipwa haki zake,” amesema Mshomba.

Mkurugenzi huyo ametaja mikakati ya baadaye ni kuimairisha kitengo cha Tehama, kuwajengea uwezo watumishi na kuweka malengo ya kutokuwa na taarifa chafu.

Akizungumza kuhusu suala la michango, Israel Mwita amesema michango inafuatiliwa kwa watumishi wanaofanya kazi za mikataba mirefu, lakini kwa mikataba mifupi inawapa shida.

Mwita amesema alikuwa akifanya kazi ya mkataba katika moja ya kampunikubwa (ameitaja kampuni hiyo), lakini baada ya mkataba wake wa mwaka mmoja kukoma, alifuatilia michango yake hakupata.

Hata hivyo, amesema baada ya kufuatilia waliungana na kutaka kufungua kesi, ndipo akaitwa yeye na wenzake wakalipwa fedha zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *