Dodoma. Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas, ameitaka Serikali kuweka mpango madhubuti kwenye makato ya fedha zinazotumwa kwa njia ya mitandao ya simu ili zisikatwe mara mbili kama ilivyo sasa.

Tarimba ametoa kauli hiyo jana, Aprili 27, 2026, alipouliza swali la nyongeza kwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, ambapo amesema mtu anayetuma mpango wa kukata fedha kwa mtumaji na kisha mpokeaji naye kukatwa si jambo jema, kwani linawaumiza wanyonge.

“Huu si mpango mzuri, mtu anayetuma fedha anakatwa, lakini anayepokea naye anakatwa, hivi hamuoni kuwa hizo ni gharama kubwa kwa mtu mnyonge anaumia? Kwa nini tusije na mpango wa kukata upande mmoja pekee?” amehoji Tarimba.

Katika swali la msingi, Tarimba alitaka kujua ni kwa nini Serikali haitoi bei elekezi kwa makato ya huduma za Mobile Money ili kuwapunguzia gharama wananchi, ambao wengi wanatumia njia hiyo.

Akijibu maswali hayo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Mussa Omar, amesema mpango wa makato kwa pande mbili utaendelea kwa sasa kwani fedha zinapotumwa pande zote mbili hunufaika.

Amesema kwa sasa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha huduma za miamala ya fedha kwa njia ya mitandao ya simu zinapatikana kwa gharama nafuu kwa wananchi.

Waziri amesema katika kipindi chote, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kupunguza gharama za miamala ya kielektroniki, kuimarisha miundombinu ya mifumo ya malipo na kuweka mazingira rafiki ya kisera na kikanuni ili kuongeza matumizi ya huduma za kifedha za kidijitali.

Kwa mujibu wa waziri, katika kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025, Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua, ikiwemo kuweka kikomo cha juu cha gharama ya muamala kwa mfumo wa malipo ya papo kwa papo na mfumo wa Tanzania Automated Clearing House (TACH) kwa miamala kati ya benki na benki, ambapo gharama ya juu kwa muamala mmoja ni Sh2,000.

“Hatua ya pili iliyochukuliwa ni kuendelea kupunguza gharama za miamala ya kutuma fedha kidijitali, ikiwamo uhamishaji wa fedha kutoka simu kwenda akaunti za benki na kutoka benki kwenda simu kupitia mfumo wa malipo madogo na ya haraka (Tanzania Instant Payment System – TIPS),” amesema Waziri.

Amesema hatua hiyo pia imepunguza gharama za miamala kwa kuwekwa ukomo wa Sh5,000 kwa miamala yote inayozidi Sh500,000, lakini kwa miamala isiyozidi kiwango hicho, mwongozo wa viwango vya juu vya gharama pia umeainishwa.

Amesema wanaendelea kutoa leseni kwa watoa huduma mbalimbali ili kuongeza ushindani katika sekta ya mifumo ya malipo ya kielektroniki, na hadi kufikia Machi 2026, jumla ya watoa huduma 113 walikuwa wamepatiwa leseni ya kutoa huduma hizo nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *