Morogoro. Tume huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) imetoa mafunzo kwa watendaji wa uchaguzi ngazi ya mkoa, Jimbo na kata watakaosimamia na kuratibu uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Isimani lililopo Halmashauri ya Wilaya ya Iringa baada ya mbunge wa Jimbo hilo Wiliam Lukuvi kufariki dunia.
Akifungua mafunzo hayo leo Jumanne, Aprili 28, 2026 Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele amesema uchaguzi huo mdogo pia utahusisha uchaguzi wa udiwani katika kata 12 ambazo ni Kata ya Mzumuni iliyopo Manispaa ya Kinondoni, Zongomera Manispaa ya Kahama, Itilo Halmashauri ya mji wa Nzega, Katare Halmashauri ya mji Tarime na Nyumlagwe Halmashauri ya Mji Kasulu.
Nyingine ni kata ya Kala iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Nkasi, Ziba Halmashauri ya wilaya ya Igunga, Kamsisi Halmashauri ya wilaya ya Mlele, Nyamugali Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Namasakata Halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Bwongera Halmashauri ya Wilaya ya Chato na Kibiti Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti.
Jaji Mwambegele amewataka wasimamizi na waratibu hao kuzingatia maelekezo watakayopewa na Tume badala ya kufanya kazi kwa mazoea na kusema kuwa kila uchaguzi unatofautiana na uchaguzi mwingine uliyopita.
Mwenyekiti wa tume huru ya Taifa ya uchaguzi Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (wa kwanza kushoto) akifuatilia mada kwenye mafunzo ya wasimamizi wa uchaguzi ngazi ya mkoa, Jimbo na kata watakaosimamia uchaguzi mdogo Jimbo la Isimani Halmashauri ya Iringa na kata 12 zilizopo kwenye Halmashauri tofauti hapa nchini, wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Tume hiyo Ramadhani Kailima. Picha Hamida Shariff
“Uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria ambazo hupaswa kufuatwa na kuzingatiwa na kwamba hatua na taratibu hizo ndio msingi wa uchaguzi kuwa mzuri na wenye ufanisi, hivyo kupunguza kama sio kuondoa kabisa malalamiko au vurugu wakati wote wa mchakato wa uchaguzi,” amesema Jaji (Rufaa) Mwambegele.
Aidha amewataka wasimamizi na waratibu wa uchaguzi huo kuvishirikisha Kwa karibu vyama vya siasa vyenye usajili kamili na wadau wengine wa uchaguzi, katika maeneo yao kuhusu masuala ya kiuchaguzi ambayo wanastahili kushirikisha kwani jambo hilo litawarahisishia utekelezaji wa majukumu yao.
Pia amewataka kuhakikisha wanayatambua na kuyajua vyema maeneo ambayo uchaguzi utaendeshwa ikiwemo miundombinu ya kufika katika vituo vya kupigia kura.
Msimamizi wa uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Jimbo la Isimani, Caroline Otieno amesema mafunzo hayo yatawakumbusha majukumu yao lakini sheria, taratibu na miongozo lengo likiwa ni kufanya uchaguzi huo kuwa huru na haki.
“Tumejipanga kwenda kusimamia uchaguzi huu bila ya kuathiri haki na maslahi ya wagombea wala sheria za uchaguzi,” amesema Otieno.
Amesema Jimbo hilo la Isimani kitahusisha kata 13 na tarafa tatu na kupitia mafunzo hayo ameahidi kuvishirikisha vyama vya siasa na kufuatia ratiba iliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Isimani katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa pamoja na kata 12 zilizopo kwenye Halmashauri mbalimbali hapa nchini wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa na tume huru ya Taifa ya uchaguzi INEC ya namna ya kuendesha uchaguzi huo. Picha Hamida Shariff
Naye Msimamizi wa uchaguzi Mkoa wa Dar es Salaam, Gerald Sondo amesema baada ya mafunzo hayo kinachofuata ni kutekeleza ratiba iliyotolewa na Tume huru ya Taifa ya uchaguzi ambapo Mei 4 hadi 10 Tume hiyo itatoa fomu za uteuzi.
Sondo amesema Mei 11 hadi 31 vyama vya siasa vitaendesha kampeni na Juni 1, uchaguzi huo mdogo utafanyika.