Tanga. Johari Mashaka alianza safari yake ya elimu mwaka 2000, akiwa na ndoto kama watoto wengine, lakini ndoto hiyo ilikatizwa ghafla na uamuzi uliomuumiza moyo.

Akiwa bado mdogo, alilazimika kuondoka shuleni alikokuwa akisoma baada ya kuambiwa hana nafasi tena kwa sababu ya ulemavu wake wa viungo kauli iliyobadilisha mwelekeo wa maisha yake na kujikuta katika sintofahamu kilichodumu kwa miaka kadhaa.

Baada ya kusoma kwa miaka mitatu katika shule ya mtaalaa wa Kiingereza (jina limehifadhiwa), Johari alifukuzwa kwa maelezo kuwa anapaswa kupelekwa katika shule maalumu za watoto wenye ulemavu.

Tukio hilo lilimlazimu kukaa nyumbani kwa takribani miaka miwili hadi mitatu huku wazazi wake wakihangaika kutafuta shule yenye miundombinu rafiki.

“Tulitafuta sana shule; kila shule tuliyopata ilikuwa haina miundombinu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, lakini wazazi wangu waliendelea kunitia moyo kuwa lazima tuendelee kutafuta shule ambayo inaweza kunipokea,” anasema Johari.

Mwangaza ulianza kuonekana siku moja baba yake alipokutana kwa bahati na wafanyakazi wa kituo cha huduma kwa watu wenye ulemavu wakati wa shughuli za kikazi. Mkutano huo uliibua matumaini mapya katika maisha ya Johari.

“Walikutana na baba wakati walipokwenda kukutana na jamii za wafugaji… hapo ndipo ulikuwa mwanzo wa maisha yangu mapya,” anakumbuka.

Baada ya maelezo hayo, Johari alipelekwa kituoni kwa ajili ya tathmini ya afya. Ilibainika kuwa alihitaji upasuaji mkubwa wa miguu. Hata hivyo, changamoto ya vifaa na utaalamu nchini ilimlazimu kupewa rufaa kwenda nje ya nchi.

“Tulivyoenda Nairobi, waliiona operesheni ni hatari na wakashauri India au Mexico kwa matibabu,” anasimulia.

Kutokana na changamoto za kifedha na maandalizi, familia ilirejea nyumbani huku wakibadilisha mkakati na kuanza tena safari ya elimu.

Johari alipata nafasi katika shule maalumu ya watoto wenye ulemavu wilayani Siha, ambako alirudia darasa la tatu na kuanza upya safari yake ya kitaaluma.

“Nilifanya usaili, nikapata nafasi, nikaanza upya darasa la tatu… Nilisoma hadi kumaliza darasa la saba,” anasema.

Katika shule hiyo, Johari alipata mazingira ya usawa na kukubalika. “Tulikuwa wanafunzi 85 wenye ulemavu; hakukuwa na unyanyapaa tulikuwa sawa.”

Baada ya elimu ya msingi, alirejea tena kwenye matibabu nje ya nchi ambako alifanyiwa upasuaji mara mbili kabla ya kurejea Tanzania kuanza elimu ya sekondari. Hata hivyo, maisha ya sekondari hayakuwa rahisi.

“Mazingira yalikuwa magumu kutoka kwa walimu hadi wanafunzi… wengi waliamini hatuwezi kufaulu,” anasema.

Changamoto za miundombinu zilimkabili kila siku; kutoka darasani hadi bweni ilikuwa safari ngumu. Licha ya hayo, alihitimu kidato cha nne mwaka 2016 na kuendelea na masomo ya uandishi wa habari katika chuo cha Arusha, ambako alipata cheti na diploma.

Ndoto yake ya kuwa mtangazaji ilikumbana na ukuta mwingine ukosefu wa miundombinu rafiki katika vyombo vya habari.

Baada ya miaka miwili ya kukaa nyumbani bila ajira, Johari aliamua kubadilisha mwelekeo na kujiunga na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, ambako alikumbana tena na changamoto zilezile.

“Nilikuwa mwanafunzi pekee mwenye ulemavu wa viungo… ilibidi baadhi ya vipindi vihamishiwe chini ili niweze kuhudhuria.”

Mwaka 2025, alihitimu shahada ya maendeleo ya jamii kwa matokeo ya kuridhisha. Hata hivyo, changamoto ya ajira bado ni kubwa kwake.

“Nafasi nyingi zinazotangazwa zinahitaji cheti au diploma… inakuwa vigumu kwangu mwenye digrii,” anasema.

Pamoja na changamoto hizo, Johari anaendelea kupambana, akisisitiza kuwa ana uwezo mkubwa wa kufanya kazi na yuko tayari kuhudumu popote atakapopata nafasi.

Katika ushauri wake kwa serikali na watunga sera, Johari anaweka wazi hitaji la mabadiliko ya kimfumo ili kuhakikisha usawa wa kweli kwa watu wenye ulemavu.

“Ningeshauri kuwe na sehemu ambayo watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele… inakuwa vigumu sisi kushindana sawa na wengine,” anasema.

Anasisitiza pia umuhimu wa miundombinu rafiki katika taasisi zote, kuanzia elimu hadi ajira, ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Aidha, anatoa shukrani kwa hatua zinazochukuliwa na serikali, lakini anaamini bado kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha sera zinageuka kuwa matendo yanayoonekana.

Anasema kwa kuwa serikali ina takwimu za watu wenye ulemavu, ni vyema zikitokea ajira walemavu wapewe kipaumbele kutokana na namna walivyopambana licha ya hali waliyonayo, badala ya kuweka mazingira ya ushindani usiozingatia uhalisia wao, hususan kwenye ajira.

“Ningeshauri wakati ajira zinapotoka serikali itupe kipaumbele. Tukiwekewa mazingira yenye usawa kati ya walemavu na wasio walemavu, sisi tunaweza kuumia zaidi,” anasema Johari.

Simulizi ya Johari ni zaidi ya hadithi ya changamoto; ni wito kwa mamlaka na watunga sera kuhakikisha hakuna mtoto anayenyimwa haki ya elimu kwa sababu ya ulemavu wake, na kila taasisi inakuwa na miundombinu jumuishi inayowezesha wote kufikia ndoto zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *