Kahama. Zaidi ya wafanyabiashara 750 katika soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, hawajalipa mapato ya Serikali tangu mwaka 2020, hali iliyosababisha halmashauri kukosa zaidi ya Sh450 milioni na kuathiri maendeleo ya soko hilo.

Wafanyabiashara hao wanaofanyia biashara juu ya meza, walitakiwa kulipa Sh10,000 kila mwezi kwa Manispaa. Kutolipa kwa muda wa takriban miaka mitano kumechangia kuongezeka kwa deni hilo kubwa.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumanne, Aprili 28, 2026, Mhasibu wa mapato wa Manispaa ya Kahama, Eliot Kalulu amesema tatizo hilo limetokana na baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kulipa kwa wakati, hali iliyosababisha madeni yao kuendelea kuongezeka.

“Hali hii imeathiri uboreshaji wa miundombinu ya soko hili lenye wafanyabiashara zaidi ya 1,000,” amesema Kalulu.

Amesema soko hilo linatumiwa pia na wakulima kutoka maeneo mbalimbali wanaoleta mazao yao.

Wafanyabiashara hao walitoa malalamiko yao katika mkutano wa mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda uliofanyika mwishoni mwa wiki ambao ulilenga kusikiliza na kutatua kero zao.

Muonekano wa eneo la ndani ya soko la Namanga katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Walilalamikia ubovu wa miundombinu huku wakidai unachangia kuwasababishia hasara, kwa kuwa magari ya mizigo hushindwa kufika ndani ya soko na hivyo kulazimika kutumia gharama zaidi kufuata bidhaa.

Baadhi yao walikiri kuwa na madeni makubwa, wakieleza kuwa moja ya changamoto ni kutoruhusiwa kulipa kwa awamu. Mfanyabiashara Hapiness John alisema hawakatai madeni yao, bali wanaomba kupewa muda zaidi na utaratibu wa kulipa kidogo kidogo.

Kwa upande wake, Jonas Mosses, mfanyabiashara wa viazi, alisema barabara za soko hilo hazipitiki kwa urahisi, hasa kwa magari makubwa ya mizigo na kuomba maboresho ya haraka ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa zao.

Naye Barnaba Paulo alisema baadhi ya wafanyabiashara wamejikuta wakirithi madeni ya wafanyabiashara waliotangulia kwenye maeneo wanayofanyia biashara, hivyo kuomba kupunguziwa adhabu ili waweze kumudu kulipa.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Florah Sangiwa akizungumzia hilo, amesema  halmashauri imeongeza muda wa ulipaji wa madeni kutoka Aprili 30 hadi Mei 30, 2026.

“Na sasa tumewaruhusu kulipa madeni yao kwa awamu,” amesema mkurugenzi huyo.

Amesema mipango ya kuboresha miundombinu ya soko tayari imeanza, ikiwemo upimaji unaofanywa na wahandisi na utekelezaji wake utategemea makusanyo ya mapato yatakayopatikana.

Muonekano wa nje eneo la vibanda katika soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya, Nkinda amewataka wafanyabiashara kulipa madeni yao ili kuiwezesha serikali kuboresha soko hilo, akisisitiza kuwa maendeleo ya miundombinu yanategemea mapato yanayokusanywa.

Amesema ni muhimu kwa wafanyabiashara kushirikiana na halmashauri kwa kulipa mapato ili kuboresha mazingira ya biashara na huduma muhimu sokoni hapo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *