MIONGONI mwa mechi kali zinazoteka hisia za mashabiki wengi hapa nchini, ni pambano linalowahusu watani wa jadi, Yanga na Simba ‘Kariakoo Derby’, kutokana na ukubwa na historia ya timu hizo kongwe hadi nje ya mipaka ya nchi.
Timu hizo kongwe zinakutana leo ikiwa ni hitimisho la fainali ya Kombe la Muungano, itakayopigwa saa 2:15 usiku, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani, Zanzibar, kabla ya kukutana tena katika Ligi Kuu Bara, Mei 3, 2026.
Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka ndani na nje ya nchi, kutokana na ukubwa na historia ya timu hizo, kisha kusubiria tena Jumapili ya Mei 3, zitakapokutana kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Yanga ilikuwa ya kwanza kuingia fainali ya Kombe la Muungano, baada ya kuifunga Azam FC mabao 2-1, katika hatua ya nusu fainali, huku kwa upande wa Simba ikifuzu kibabe pia kwa kuichapa Mlandege 3-0.
Wakati timu hizo zikikutana, rekodi zinaibeba Simba ikicheza Zanzibar katika michuano mbalimbali tofauti na wapinzani wake, imeshinda mechi nne, huku Yanga ikishinda mbili na mara moja hakukuwa na mbabe.
Mechi ya leo ni ya nane kukutana visiwani huko na Mwanaspoti linakuelezea zilipokutana na matokeo jinsi yalivyokuwa baina yao.
JANUARI 1975
Hili ndilo lililokuwa pambano la kwanza kwa Simba na Yanga kukutana visiwani katika fainali za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Sasa Kombe la Kagame) iliyofanyika Zanzibar na Yanga ilishinda mabao 2-0.
Michuano hiyo ilishirikisha timu sita, Simba, Gor Mahia FC ya Kenya na Jeshi ya visiwani Zanzibar zilizokuwa Kundi A, huku Mufulira Wanderers ya Zambia, Express ya Uganda na Yanga zikipangwa Kundi B.
Michuano hiyo iliyokuwa na ushindani ilishuhudiwa Simba na Gor Mahia za Kundi A zikitinga nusu fainali, huku Yanga na Mufulira zikifanya hivyo kutoka kundi B.
Simba ilitinga fainali kwa kuifunga Mufulira mabao 2-0 na Yanga kuichapa Gor Mahia ‘K’Ogalo’ bao 1-0.
Katika fainali mabao ya Yanga yalifungwa na Gibson Sembuli na Sunday Manara ‘Computer’.
JANUARI 1992
Baada ya miaka 17 kupita, timu hizo zikakutana tena Zanzibar, katika fainali kwenye michuano hiyo iliyoshirikisha timu saba, ambazo ni Bata Bullets (kwa sasa Nyasa Big Bullets FC) ya Malawi, Simba, Al Hilal ya Sudan na Jamhuri ya Zanzibar zilizokuwa Kundi B, huku Yanga ikipangwa Kundi A na Small Simba ya Zanzibar na Rivatex FC ya Kenya.
Yanga na Small Simba zilikwenda nusu fainali Kundi A, huku Simba na Al Hilal zikipenya Kundi B na katika hatua hiyo, Simba iliinyoa Small Simba bao 1-0 na Yanga kuichapa Al Hilal kwa penalti 10-9, baada ya mechi kuisha kwa suluhu (0-0).
Katika fainali Simba ilitwaa ubingwa kwa kuifunga Yanga penalti 5-4, baada ya miamba hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, dakika za kawaida.
Penalti za Simba zilipigwa na George Masatu, Hamza Maneno, Fikiri Magosso, Issa Kihange na George Lucas ‘Gaza’, huku Twaha Hamidu maarufu ‘Noriega’, Kassongo Athuman na Damian Kimti wakikosa.
Penalti za Yanga zilifungwa na Said Mwaibambe ‘Zimbwe’, Issa Athuman, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’, huku Said Mwamba ‘Kizota’, Salum Kabunda ‘Ninja’, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na David Mwakalebela wakikosa.
OKTOBA 27, 1992
Jumanne ya Oktoba 27, 1992, timu hizo zilikutana tena, ingawa, safari hii ni kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Muungano, ikiwa ni takribani miezi tisa imepita tangu Simba ishinde ubingwa wa Klabu Bingwa Cecafa.
Simba ilishinda bao 1-0 la Damian Kimti na kupeleka kilio Yanga iliyotoka kuchapwa pia kwenye Ligi Kuu mabao 2-0, Septemba 26, 1992.
Awali Yanga ilishinda mechi ya kwanza ya Ligi ya Bara bao 1-0 lililotokana na shuti kali la mbali la beki, Kenneth Mkapa dakika ya 10, kisha kudumu hadi dakika ya mwisho ya mechi, pambano lililopigwa Jumapili ya Aprili 12, 1992.
JANUARI 12, 2011
Mechi ya nne kwa timu hizo kukutana Zanzibar ni ya fainali ya Michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopigwa Januari 12, 2011, ikiwa ni siku ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mechi hiyo ya kwanza kwa vigogo hao kukutana katika Michuano ya Mapinduzi, mabao ya Simba yalifungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ dakika ya 33 na Shijja Mkina dakika ya 71, huku Yanga ikichezesha asimilia kubwa ya kikosi cha wachezaji vijana.
JANUARI 10, 2017
Kariakoo Derby ya tano kupigwa visiwani ilipigwa Januari 10, 2017, ikiwa ni nusu fainali ya Michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 na Simba iliifunga Yanga kwa penalti 4-2, baada ya dakika 90, kumalizika kwa suluhu (0-0).
Penalti za Simba zilizofungwa na aliyekuwa nahodha wa kikosi hicho kwa wakati huo, Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Mzamiru Yassin na Javier Besala Bokungu, huku, Method Mwanjali akikosa.
Kwa upande wa Yanga zilifungwa na Simon Msuva na Thabani Kamusoko, huku za Haji Mwinyi Mngwali na kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ zikiokolewa na kipa wa Simba na kuivusha timu hiyo kwenda fainali ilipokabiliana na Azam FC.
Katika fainali ya mwaka 2017, Simba ilichapwa bao 1-0 na Azam FC, lililofungwa kwa shuti kali na kiungo nyota wa timu hiyo, Himid Mao Mkami ‘Ninja’ dakika ya 13, hivyo kutwaa ubingwa huo uliokuwa wa tatu kwao.
JANUARI 13, 2021
Mechi hii ilikuwa ni ya fainali ya Kombe la Mapinduzi na Yanga ilishinda kwa penalti 4-3, baada ya dakika zote 90, kumalizika kwa suluhu (0-0), hivyo, kubeba ubingwa huo ukiwa ni wa pili tangu mara ya mwisho ilipochukua mwaka 2007, ilipoichapa Mtibwa Sugar mabao 2-1.
Penalti za Yanga zilifungwa na Tuisila Kisinda ‘TK Master’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Zawadi Mauya na Saidi Ntibazonkiza ‘Saido, huku Mkongomani Mukoko Tonombe, akikosa mbele ya kipa Beno Kakolanya.
Kwa upande wa penalti hizo tatu za Simba, zilifungwa na Francis Kahata, Chris Mugalu na Gadiel Michael, huku waliokosa ni Meddie Kagere iliyogonga mwamba na ya Joash Onyango ikiokolewa na Farouk Shikalo.
MACHI 1, 2026
Hili lilikuwa ni pambano la kwanza la Ligi Kuu kwa msimu wa 2025-2026, kukutana kwa miamba hii katika mechi ya ‘Kariakoo Derby’, likiwa ni la 115, tangu mwaka 1965 na lilipigwa Zanzibar kwa mara ya kwanza Machi 1, 2026.
Katika mechi zilitoka suluhu ya (0-0), ikiwa ni sare ya kwanza kwa Simba tangu mara ya mwisho ilipoifunga Yanga mabao 2-0, Aprili 16, 2023.
APRILI 29, 2026
Baada ya kupita siku 59, tangu zilipokutana Machi 1, 2026, miamba hii inakutana tena leo Aprili 29, 2026, ingawa, safari hii ni katika mechi ya fainali ya Kombe la Muungano, kabla ya kukutana kwenye Ligi Kuu Bara raundi ya pili, Mei 3, 2026.
Yanga inaingia na kumbukumbu nzuri baada ya kutwaa taji hilo la Kombe la Muungano mwaka 2025 kwa kuifunga JKU FC bao 1-0, lililofungwa na Maxi Nzengeli, katika fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, Mei 1, 2025.
Rekodi zinaonyesha, Yanga ndiyo timu iliyotwaa taji hilo mara nyingi, ikifanya hivyo mara saba, kuanzia mwaka 1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000 na 2025, ikifuatiwa na Simba iliyotwaa mara sita, 1993, 1994, 1995, 2001, 2002 na 2024.
Mara ya mwisho Simba kutwaa taji hilo ni mwaka 2024, ilipoichapa Azam FC bao 1-0, la aliyekuwa kiungo wake, Babacar Sarr dakika ya 77 na kuipa ubingwa huo wa sita, chini ya kocha mkuu wa zamani wa kikosi hicho, Mualgeria Abdelhak Benchikha.
Ubingwa huo pia ulikuwa pia ni wa kwanza kwa kikosi hicho, tangu michuano ya Kombe la Muungano iliporejea tena, baada ya kushindwa kufanyika kwa kipindi cha miaka 22, tangu mara ya mwisho ilipofanyika mwaka 2002.
Ikiwa Yanga itashinda, itakuwa ni taji lake la nane na kuifanya kuzidi kuweka rekodi ya kuongoza kwa kutwaa mara nyingi zaidi na endapo Simba itaibuka kidedea itaifikia rekodi ya kikosi hicho cha mitaa ya Jangwani.
MABINGWA WA LIGI YA MUUNGANO TANGU ILIPOANZA RASMI 1982
7-Yanga (1983, 1987, 1991, 1996, 1997, 2000, 2025)
6-Simba (1993, 1994, 1995, 2001, 2002, 2024)
3-Majimaji (1985, 1986, 1998)
2-Malindi (1989, 1992)
1-Pan Africans (1982)
-KMKM (1984)
-African Sports (1988)
-Pamba (1990)
-TZ Prisons (1999)
(N:B)-Michuano hii ilirejea tena mwaka 2024, baada ya kutofanyika kwa kipindi cha miaka 22, tangu mara ya mwisho ilipofanyika 2002.