
UPEPO haupo vizuri kwa beki wa kulia wa Yanga, Israel Mwenda na wakati wowote mwisho wa msimu huu linaweza kutokea kwa kuondoka huku Simba ikitajwa.
Kuanzia mwanzo wa msimu huu, Mwenda alikuwa beki tegemeo wa Yanga akionyesha uwezo mkubwa lakini ghafla baada ya mchezo wa marudiano wa mzunguko wa pili kati ya timu hiyo dhidi ya Simba mambo yamebadilika sana.
Mwenda kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, beki huyo alikuwa akiandamwa na mashabiki wa klabu hiyo, akionekana kama makosa makubwa yalianzia kwake wakati wekundu hao wakitengeneza bao la kwanza.
Kuanzia hapo beki mwenzake Yao Kouassi akaanza kurudi kwenye kikosi cha kwanza licha ya kwamba Mwenda alikuwa chaguo la kwanza kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Pedro Goncalves.
Kabla ya mchezo huo wa Simba ambao Mwenda alicheza dakika 45 za kwanza pekee, beki huyo alikuwa chaguo a kwanza kwenye kikosi hicho akicheza jumla ya dakika 1545 za mechi za ligi pekee, akikosa mechi sita pekee.
Msimu huu Mwenda licha ya kucheza mechi nyingi alifanikiwa kutengeneza asisti tatu pekee lakini akiwa ndio beki wa kulia aliyetengeneza asisti nyingi.
“Kuna uwezekano mdogo wa Mwenda kubaki na sisi kwa msimu ujao, kuna mambo kuanzia ule mchezo wa Simba hatuyaelewi kutokana na kiwango chake,’’ alisema bosi huyo.
“Bado tunaendelea kumtafakari sana lakini kwa sasa tunaona ni bora aendelee kucheza Yao kwanza wakati tunatafuta uhalisia wa wasiwasi wetu juu yake.
Yanga mpaka jana asubuhi ilikuwa tayari mkoani Kigoma tayari kwa mchezo wa ligi wa ugenini dhidi ya Mashujaa ya huko lakini Mwenda hakuwa sehemu ya msafara huo.
“Hata huku Kigoma, hakuja na timu na hatuna taarifa zake labda kwa uongozi wa juu kabisa watakuwa wanajua lakini sio makocha wala sisi wengine.
SINGIDA YATAJWA
Yanga inaelezwa kwamba Mwenda huenda akapelekwa Singida Black Stars kwa msimu ujao kutokana na kwamba bado ana mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa hao.
Yanga ilimsajili Mwenda akitokea Singida ambapo awali alisaini mkataba wa mkopo wa miezi sita kabla ya baadaye kusaini mkataba kamili na Mabingwa hao wa miaka miwili, akiwa ndio kwanza alikuwa anamalizia mwaka wa kwanza msimu huu.
Simba uliwahi kumpigia hesabu za kumrudisha Mwenda lakini dili hilo lilikwama kutokana na beki huyo hapatani na mwenzake mmoja mkongwe aliyepo ndani ya kikosi cha wekundu hao.
