Dar es Salaam. Katika kukomesha ndoa za utotoni pamoja na mila na desturi kandamizi kama ukeketaji jamii zinazotekeleza hayo zimetakiwa kuacha kwani kufanya hivyo kunamuumiza mtoto hasa wa kike.

Katika hilo watoto wametakiwa kuishi kama watoto na si kubebeshwa majukumu mazito ya ndoa na maumivu yatakayowatesa katika maisha yao.

Kauli hiyo imetoka kwa Wakili Irene Nambuo, ofisa uchechemuzi Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF) ambalo ni sekretarieti ya Mtandao wa Kutokomeza Ndoa za Utotoni Tanzania (TECMN), katika semina ya mafunzo maalumu kwa waaandishi wa habari yenye lengo la kuongeza uelewa wa namna ya kuandika na kuripoti taarifa kuhusu ulinzi wa mtoto makao makuu ya CDF jijini Dar es Salaam.

“Tusiwatwishe majukumu ya kiutuuzima kama ndoa, wanatakiwa wafurahie utoto wao na wapate nafasi ya kufanya uamuzi wao wenyewe, wapate elimu ili tusitengeneze jamii tegemezi,” amesema Irene ambaye pia ni mratibu wa TECMN.

Ikumbukwe, Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 inaruhusu mvulana kuoa kuanzia umri wa miaka 18, na msichana kuolewa kuanzia miaka 14 na miaka 15 kwa kibali cha wazazi, ambapo wadau wamekuwa wakipigia kelele sheria hiyo wakisema inamnyima mtoto wa kike haki zake za msingi hasa haki ya kupata elimu.

Ofisa uwezeshaji wa wasichana shirika la CDF Lilian Kimath, amesema wamejikitia katika kuwatengenezea uwezo wasichana ili waweze kuondokana na changamoto hizo.

“Katika miaka 20 tuliyofanya kazi tumefanikiwa kuwafikia wasichana takribani 2000,” amesema.

Amesema pia wamejenga madawati ya kijinsia katika mikoa ya Manyara, Serengeti na Butiama ili vitendo vya kikatili viweze kushughulikiwa kwa wakati na huduma kuwa karibu na jamii.

“Tupitia miradi yetu ya vijana tumeweza kuwafikia vijana 6577 kwa upande wa Tarime ili kuhakikisha tunapunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi,” amebainisha.

Akielezea changamoto Lilian amesema sera na sheria bado hazifanyiwi kazi hususani kwenye maeneo ya jamii ambayo ni vigumu kufikika.

“Baadhi ya wazazi kutokuwa na uelewa mzuri wa ulinzi wa mtoto na mila na desturi kandamizi ambazo bado zinang’ang’aniwa na baadhi ya watu jambo ambalo linarhdisha nyuma juhudi,” amesema.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika CDF, Irene Ernest amesema wanazo programu za kuhakikisha mtoto analindwa ambazo zinatekelezwa akitolea mfano uwepo wa klabu za shuleni za watoto kujifunza namna ya kujilinda.

Hata hivyo, katika kukomesha changamoto hizo juhudi zimekua zikifanyika ikiwemo kutaka kubadilisha sheria hiyo ambayo itakua umri wa kuolewa ni miaka kuanzia 18 na si chini ya hapo.

Irene amesema juhudi na mikakati kwa kushirikiana na taasisi, wizara mbalimbali kama Katiba na Sheria, Maendeleo ya Jamii na Elimu kuona namna ya kushirikiana ili kubadilisha sheria hiyo pamoja na uchechemuzi wa sera.

Kwa upande wa waandishi wa habari wamesisitizwa kuendelea kuwa nguzo muhimu ya ulinzi wa mtoto kama kuzingatia maadili ya taaluma yao wakati wa uripotiji taariza za watoto .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *