Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imetahadharisha kuhusu hatua zozote za uchokozi na ukatili za serikali ya Trump katika Ghuba ya Uajemi na kutangaza kuwa Sana’a inaunga mkono hatua za Iran katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen ilisisitiza Jumanne katika taarifa yake kwamba uchokozi wa Marekani na utawala wa Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na uharamia wa Marekani katika Bahari ya Oman umeilazimisha dunia kulipa gharama kubwa, hatua ambazo zimesababisha  kuvurugika kwa minyororo ya usambazaji na usafiri wa baharini na kupanda gharama za usafiri na bei za nishati na chakula duniani.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen imelaani uharamia wa Marekani katika Bahari ya Oman na mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara za Iran na kukamatwa kwa wafanyakazi wa meli hizo, na kuitaja hatua hiyo kuwa ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na uhuru wa safari za meli.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Yemen pia imesema kuwa hatua zote zinazochukuliwa na Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz na kuwa na haki ya kujilinda na kuzuia safari za meli katika maji yake ili kukabiliana na vitisho vya usalama ni halali, na kusisitiza kuwa njia pekee ya kupatia ufumbuzi hali ya mambo katika Mlango-Bahari wa Hormuz ni kushughulikia chanzo cha uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *