MAREKANI: Serikali ya Tanzania imeeleza mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuimarisha ustawi na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu, huku ikisisitiza umuhimu wa kuongeza upatikanaji wa vifaa na teknolojia saidizi ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akihitimisha ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu (COSP19-CRPD) uliofanyika New York, Marekani, Juni 11, 2026, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema teknolojia na vifaa saidizi vina mchango mkubwa katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii.
“Ni muhimu kuendelea kuongeza upatikanaji na matumizi ya vifaa na teknolojia saidizi kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa usawa pia Serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo dhana ya ujumuishwaji kwa kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa na haki kwa usawa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” amesema Mahundi.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Naibu Katibu Mkuu, Dk. James Kilabuko, amesema ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo umeiwezesha nchi kujifunza uzoefu na mbinu mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika uwezeshaji na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu hivyo Kupitia mkutano huu, tumejifunza mbinu na uzoefu kutoka mataifa mbalimbali ambazo zitatusaidia kuimarisha zaidi juhudi zetu, lakini pia Serikali itaandaa mpango kazi mahususi kwa kushirikiana na wizara, taasisi na wadau mbalimbali ili kuendeleza utekelezaji wa masuala ya watu wenye ulemavu na kushughulikia changamoto zilizobainishwa wakati wa mkutano huu,” amesema Dk. Kilabuko.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Grace Maghembe, amesema Tanzania imeendelea kuboresha huduma za afya za msingi kwa watu wenye ulemavu kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kuanzia ngazi ya jamii, sambamba na kuboresha miundombinu ya afya na kuwajengea uwezo watumishi wa sekta hiyo katika utoaji wa huduma jumuishi.

Aidha, ameshauri Shirika la Afya Duniani (WHO) kuangalia uwezekano wa kutumia mifumo inayotumika katika upatikanaji wa chanjo na dawa muhimu duniani ili kuboresha upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu, hususan katika nchi zinazoendelea.
Mkutano wa COSP19 umezikutanisha nchi wanachama wa Mkataba wa haki za Watu Wenye Ulemavu kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuimarisha haki, ushiriki na ustawi wa watu wenye ulemavu duniani.a