Katika jitihada za kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa kundi kubwa la vijana ambao kimsingi ndiyo nguvu kazi ya Taifa, Mantra Tanzania Limited inaendelea kutoa mafunzo mahususi ya kuwawezesha vijana kupata ujuzi unaohitajika ili waziendee fursa za ajira za wazi zilizopo katika mradi wa Mto Mkuju uliopo Mkoa wa Ruvuma, kusini mwa Tanzania.
Mradi wa Mto Mkuju unahusika na utafiti na uchimbaji wa madini ya urani, unaofanyika katika Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma.
Kampuni hiyo hivi karibuni imewapokea waendesha mitambo 10 wapya waliopata mafunzo ili kushiriki katika awamu inayofuatia ya maendeleo ya mradi, hatua inayodhihirisha mafanikio makubwa katika kuwainua wazawa.
Waendesha mitambo hao, walioajiriwa kutoka Wilaya ya Namtumbo, wana ujuzi wa kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa vinavyotumika katika shughuli wa uchimbaji wa madini hayo. Kujumuishwa kwao katika shughuli za uendeshaji kunaonyesha mkakati madhubuti wa kampuni hiyo wa kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, inayotegemewa na inayotokana na jamii wenyeji ili kusaidia utekelezaji wa moja ya miradi muhimu ya nishati nchini Tanzania.
Kipaumbele kikubwa kimewekwa kwenye upatikanaji wa rasilimali watu walio tayari na wenye ujuzi, mradi huo unapoelekea katika hatua ya ujenzi wa miundombinu ya kuchakata madini ya urani.
Upatikanaji wa waendeshaji mitambo wazawa waliopata mafunzo unatarajiwa kuharakisha utekelezaji wa mradi, kuongeza ufanisi wa gharama, na kuhakikisha shughuli za uendeshaji hazisimami kwa ujumla, jambo linaloonyesha umuhimu wa kuwa na vijana wazawa wenye uwezo mkubwa.
“Mafanikio haya yanaakisi njia thabiti tulizoamua kuzipita hadi kufanikiwa kuendeleza mradi ikiwemo kuwekeza mapema katika rasilimali watu, mifumo na maarifa yatakayohakikisha ufanisi na uendelevu wa shughuli za mradi kwa kiwango kikubwa,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Mantra Tanzania Limited, Illya Shchukin.
“Kwa kuweka kipaumbele kwenye kuchukua vijana wazawa wenye uwezo, kwa kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kazi na mamlaka za uhamiaji chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, tunaimarisha utii wa sheria, kuboresha mipango ya rasilimali watu, na kuhakikisha mradi wa Mto Mkuju unakuwa na manufaa ya muda mrefu kwa wadau wetu na jamii za Wilaya ya Namtumbo.”
Kuajiri vijana wazawa wenye uwezo imekuwa faida kubwa hususan katika miradi mikubwa ya rasilimali. Kwa kuwekeza mapema katika mafunzo ya ufundi stadi na mifumo ya ajira, Mantra Tanzania Limited inauweka mradi wa Mto Mkuju katika nafasi nzuri ya kupunguza changamoto zinazohusiana na ukosefu wa ajira, gharama kubwa za wataalamu kutoka nje, na pia kukuza ustawi wa jamii kwa njia ya kuwaongezea kipato.
Mradi huu unatekelezwa kwa mujibu wa kanuni za kimataifa na sheria za mamlaka za Tanzania, ikiwemo Wizara ya Madini na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, na kuhakikisha viwango vya kimataifa katika maendeleo ya urani vinazingatiwa. Uhakiki huu wa taratibu unatoa uhakikisho wa kisheria na kuishikilia imani ya wawekezaji katika mradi huo.
Ukiachilia mbali masuala ya kisheria na taratibu, mkakati wa kampuni hiyo wa rasilimali watu umesaidia kuweka mazingira bora ya kiuendeshaji. Ajira kwa wazawa na uhamishaji wa ujuzi ni vichocheo muhimu vya matumaini na msaada kwa jamii, kupunguza hatari za kijamii na kuupa mradi uhai wa muda mrefu.
Meneja Uendelevu, Bw. Majani Moremi anasema: “Hapa Mantra, tunapozungumzia uchimbaji endelevu hauishii kwenye uhifadhi wa mazingira na uwekezaji kwa jamii tu, bali pia inahusu kuleta manufaa endelevu kwa jamii. Kwa kuwapatia vijana wazawa ujuzi wa kisasa na muhimu na kushiriki katika mradi wa Mto Mkuju, tunaimarisha uaminifu wa jamii kwetu pamoja na utayari na ufanisi wa kiuendeshaji.”
Kundi hili ni sehemu ya mpango maalumu wa maendeleo ya rasilimali watu uliobuniwa kusaidia upanuzi wa shughuli za uendeshaji huku ukidumisha viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama na utendaji.
Kuajiriwa kwa waendeshaji mitambo hawa, ni hatua ya awali ya mpango mpana wa maendeleo ya nguvu kazi unaoendana na mzunguko wa maisha ya mradi. Kadri mradi unavyopiga hatua, Mantra Tanzania Limited inaendelea kutoa mafunzo na kuendesha programu za ajira ili kuhakikisha sehemu kubwa ya wafanyakazi inatoka ndani ya nchi na ina ujuzi wa kitaalamu.
Kwa mtazamo wa wawekezaji, mbinu hii inaimarisha uwezo wa utekelezaji mradi huku ikiendana na matarajio ya kimataifa ya Uwajibikaji, Uendelevu na Maadili ya Uongozi. Inaonyesha uwiano sahihi kati ya ufanisi wa kiuendeshaji, uzingatiaji wa sheria na ushirikishwaji wa wadau, ambavyo ni nguzo muhimu kwenye kuleta manufaa ya muda mrefu ya mradi.
Wakati Tanzania ikiendelea kujipanga katika mnyororo wa thamani wa nishati ya nyuklia duniani, mradi wa Mto Mkuju unasimama kama rasilimali ya kimkakati, huku uwekezaji wa Kampuni hii katika rasilimali watu ukiimarisha matumaini, imani na utayari wa kutoa matokeo endelevu kwa manufaa ya Taifa na wananchi wake.
Kubadilisha maisha kupitia ujuzi na ajira
Kwa waajiriwa wengi wapya, fursa hii ni mwanzo mpya wa maisha yao.
“Fursa hii itabadilisha maisha yangu na ya familia yangu. Kwa ujuzi wa vitendo nilionao, nitaongeza kipato changu na kutoa msaada kwa ndugu zangu,” alisema Hassan Salehe Mabukusela kutoka Kijiji cha Likuyu.
Mabukusela, mwenye umri wa miaka 28 na mhitimu wa chuo kikuu, ni miongoni mwa waajiriwa wapya wanaosaidia kazi katika awamu nyingine ya utekelezaji wa mradi wa Mto Mkuju.
Anaeleza kuwa sasa ana ujuzi wa kutumia teknolojia ya kisasa na kufuata viwango vya usalama kazini. Kabla ya kupata fursa ya ajira kwenye mradi, Mabukusela alikuwa akijishughulisha na kazi ndogondogo nyumbani kwao.
“Sasa nimepata mafunzo ya kutosha na niko tayari kufanya kazi katika mazingira ya kisasa na ya kitaalamu ya uchimbaji,” alisema.
Mbali na ajira, yeye na familia yake sasa wana uhakika wa kipato chao na wanashiriki katika shughuli za maendeleo ya jamii.
“Hii si kwa ajili yangu tu, bali pia kwa familia yangu na kuwasaidia wengine kuona inawezekana.”
Kujenga kujiamini na dhamira
Mwajiriwa mwingine, Kubri Mustafa kutoka Kijiji cha Mtonya, anasema mafunzo hayo yamemjengea kujiamini na kumpa mwelekeo mpya wa maisha.
Aliongeza kuwa, fursa hiyo imemwezesha kupata ujuzi wa vitendo na uwezo wa kuchangia kikamilifu katika jamii yake na Tanzania kwa ujumla.
Mustafa anajisikia fahari kuwa sehemu ya watu wanaochangia maendeleo ya sekta ya nishati hususan madini ya urani nchini.
“Ninatarajia kuwa mtaalamu wa uchimbaji wa urani nchini Tanzania na barani Afrika.”