
Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Afya Duniani WHO, World Health Summit, Chuo Kikuu cha Aga Khan pamoja na Wizara ya Afya ya Kenya na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Washiriki wamejadili changamoto za ongezeko la magonjwa sugu, mabadiliko ya magonjwa ya kuambukiza, ufadhili wa afya na matumizi ya teknolojia katika kukabiliana na dharura za kiafya.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO, Mohamed Janabi amesema bara la Afrika linahitaji mshikamano na hatua za pamoja katika kuimarisha huduma za afya.
Ameongeza kuwa katika siku hizi tatu tumeimarisha ushahidi na dhamira yetu. Tunaondoka hapa na ahadi za kikanda zenye malengo ya kimataifa.
Kwa upande wake, Rais wa mkutano huo, Lukoye Atwoli amesema mkutano huo umejikita katika masuala muhimu yanayoathiri afya ya Waafrika sasa na siku zijazo.
Mkutano huo pia umeonesha ubunifu mbalimbali wa WHO ikiwemo teknolojia ya akili Mnemba kwa ajili ya kukabiliana na dharura za kiafya pamoja na mfumo wa uhalisia pepe unaoiga zoezi la chanjo dhidi ya polio katika jamii.