Siku hiyo, itayoadhimishwa kila mwaka Aprili 29 kufuatia azimio la mwaka 2025 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, inalenga kuwaenzi mamilioni ya watu waliopoteza maisha au makazi yao kutokana na matetemeko ya ardhi na kuhimiza hatua za kuzuia madhara na maendeleo yanayozingatia hatari.

Matetemeko hayaepukiki, lakini maafa yake yanaweza kuzuilika: Guterres

Katika ujumbe wake wa siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameonya kuwa matetemeko ya ardhi bado ni miongoni mwa majanga hatari zaidi ya asili duniani.

“Matetemeko ya ardhi ni miongoni mwa majanga mabaya zaidi ya asili. Kwa sekunde chache tu, yanaweza kubadili nyumba kuwa magofu, kufuta maendeleo ya miongo kadhaa na kusababisha vifo vya maelfu ya watu,” amesema.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa sheria madhubuti za ujenzi, mazoezi ya mara kwa mara ya dharura na mipango bora ya miji ni muhimu katika kulinda jamii zilizo hatarini.

“Matetemeko ya ardhi hayaepukiki, lakini maafa yake yanaweza kuzuilika,” ameongeza Guterres. “Kwa maandalizi na mipango sahihi, tunaweza kujenga miji na jamii salama zaidi hata ardhi inapoyumba kwa nguvu.”

© UNICEF UNICEF inazisaidia familia zilizoathiriwa na tetemeko la ardhi lililotokea kaskazini mwa Afghanistan. (Maktaba)

Majanga ya hivi karibuni yaonesha dunia bado iko hatarini

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kushuhudia athari kubwa za matetemeko ya ardhi katika mataifa kama Myanmar na Afghanistan, ambako matetemeko ya hivi karibuni yamesambaratisha nyumba, miundombinu na kusababisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupunguza Hatari za Majanga (UNDRR), matetemeko ya ardhi yamesababisha baadhi ya vifo vikubwa zaidi vya majanga katika historia ya kisasa.

Tangu mwaka 1900, takriban matetemeko 12 makubwa yamesababisha kila moja vifo vya zaidi ya watu 50,000.

Mbali na kupoteza maisha, matetemeko hayo pia husababisha hasara kubwa za kiuchumi. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa majanga ya matetemeko yanachangia zaidi ya robo ya hasara zote za majanga duniani, huku yakisababisha uharibifu wa matrilioni ya dola katika miongo ya hivi karibuni.

Wataalamu wanaonya kuwa madhara hayo hayaishii kwenye majengo kubomoka pekee, kwani matetemeko yanaweza pia kusababisha tsunami, moto na maporomoko ya ardhi yanayoharibu makazi, huduma za afya, shule na vyanzo vya maisha.

Umaskini na miundombinu dhaifu vinaongeza hatari

UNDRR imesema hatari ya matetemeko ya ardhi inaongezeka kutokana na ukuaji wa haraka wa miji katika maeneo yenye mitetemeko, miundombinu chakavu, umaskini, ukosefu wa usawa na kutotekelezwa ipasavyo kwa sheria za ujenzi.

Shirika hilo limeeleza kuwa uwekezaji katika miundombinu imara na sera za maendeleo zinazozingatia hatari ni muhimu katika kupunguza madhara ya baadaye.

Siku hiyo ya Kimataifa pia inalenga kuhamasisha utekelezaji wa vipaumbele vya Mfumo wa Sendai wa Kupunguza Hatari za Majanga, makubaliano ya kimataifa yanayolenga kuzuia hatari mpya za majanga na kupunguza zilizopo kupitia maandalizi na ujenzi wenye mnepo.

“Tahadhari madhubuti kuanzia mazoezi ya mara kwa mara, sheria kali za ujenzi hadi upangaji bora wa miji  ni muhimu katika kulinda jamii,” amesema Guterres huku akisisitiza kuwa mshikamano wa kimataifa ni muhimu katika kukabiliana na majanga na kuisaidia jamii kupona baada ya maafa.

© UNFPA Wasichana nchini Nepal.

Kuwakumbuka waathirika huku dunia ikijiandaa kwa siku zijazo

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema maadhimisho hayo ya kila mwaka hayalengi tu kuwakumbuka waliopoteza maisha, bali pia kuhamasisha serikali, wahandisi, wapangaji wa miji na jamii kuchukua hatua kabla ya majanga kutokea.

Kwa kuwa mamilioni ya watu duniani wanaishi katika maeneo yanayokumbwa na matetemeko ya ardhi, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa maandalizi yanaweza kuwa tofauti kati ya maisha na maafa.

Kadri shughuli za kumbukumbu na kampeni za uhamasishaji zilivyoendelea duniani kote, ujumbe wa Umoja wa Mataifa umeendelea kuwa mmoja, ingawa matetemeko ya ardhi hayawezi kuzuiwa, vifo na uharibifu mkubwa unaotokana nayo unaweza kupunguzwa kupitia maandalizi, kujenga mnepo na mshikamano wa pamoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *